Wednesday, December 21, 2011

Bodi ya Chakula Zanzibar yakamata Tende ‘Feki’

BODI ya Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar imefanikiwa kukamata tani mbili za tende zilizokwisha muda wake katika maghala mawili Mjini Zanzibar.Tende hizo zimegunduliwa zikiuzwa na wafanyabiashara wadogo wadogo (wamachinga) katika maeneo ya Darajani kwa bei ya Sh500 kwa nusu kilo na kupigwa Muhuri wa bandia kuwa zinafikia kikomo cha matumizi yake mwaka 2012.

Ukamatwaji wa tende hizo unatokana na Operesheni ya kukagua bidhaa katika Mabucha mbali mbali ya Nyama kulikofanywa na Bodi hiyo jana katika maeneo mbali mbali ya Mjini Zanzibar.

Mrajis wa Bodi ya Chakula , Dawa na Vipodozi Zanzibar, Dk Burhan Othman Simai amesema kuwa baada ya kuwakamata wafanyabiashara hao waliwapeleka katika kituo cha polisi na kuweza kusaidia kuonesha sehemu walikozipata tende hizo.

Amesema Maghala yaliyogundulika ni pamoja na Ghala la Malindi linalomilikiwa na Ali Amour Mohammed na Ghala la Kwa Haji Tumbo linalomilikiwa na Mohammed Abdalla Rashid.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mrajis amesema , Tende hizo ambazo zimekwisha muda wake wa Matumizi zinatarajiwa kuangamizwa hivi karibuni ambapo gharama za uangamizaji wa bidhaa hiyo zitatolewa na wamiliki wa bidhaa hiyo.

Aidha katika Operesheni hiyo BODI ya Chakula, Dawa na Vipodozi imebaini kasoro mbali mbali zikiwemo zile zinazohatarisha afya ya binadamu.
Katika kupambana na hali hiyo amesema hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuyafungia baadhi ya mabucha na kuwafungulia mashtaka wauzaji 36 wa nyama katika maeneo mbali mbali ya Unguja.

Dk Burhan amefahamisha kuwa Bodi hiyo imedhamiria kufanya operesheni maalum na kubwa hivi karibuni ambayo itakagua mabucha yote, sehemu za kuuzia bidhaa za mifugo pamoja na machinjio kwa upande wa Unguja na Pemba. Ukaguzi huo utajumuisha Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Jeshi la Polisi.

No comments:

Post a Comment