Friday, December 30, 2011

POLISI ZANZIBAR WAZIMA JARIBIO KUBWA LA UJAMBAZI

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, limefanikiwa kuzima jaribio kubwa la ujambazi lilokuwa lifanyike mara baada ya kuchukuliwa kwa mishahara ya watumishi wa hoteli moja ya Kitalii.
Afisa Habari wa Jeshi hilo Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema kuwa jaribio hilo limezimwa na Polisi jana Alhamisi Desemba 29, 2011 majira ya saa 7.00 mchana baada ya makachero wa Jeshi la Polisi kupata taarifa mapema na kuweka mtego uliowanasa majambazi watatu kati ya sita.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed, amesema kuwa majambazi wapatao sita wakiwa na silaha aina ya SMG walijipanga kumteka mhasibu wa Hoteli ya Kitalii ya Blue Bay iliopo Kiwengwa huko Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kamanda Aziz amesema majambazi huo walipanga kufanyika uporaji huo mara baada ya kuchukuliwa kwa mishahara hiyo ya watumishi wa Hoteli ya Blue Bay na tukio hilo lingefanyika njiani wakati mhasibu huyo akitokea katika Tawi la Benki ya Barclays lililopo eneo la Kinazini Mjini Zanzibar na Hoteli ya Blue Bay ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema majambazi hayo yalifika eneo la tukio wengine wakiwa kwenye gari dogo na wengine wakiwa kwenye pikipiki za kukodi mbili za kukodi vyombo ambavyo viliegeshwa pembeni mwa barabara inayoelekea Bububu wakimsubiri Muhasibu wa Hoteli ya Blue Bay atoke Benki ili wampore fedha hizo ambazo zilikuwa za kigeni.
Hata hivyo Kamanda Aziz amesema kuwa katika tukio hilo ulifanyika ukamataji salama ambao haukuhusisha matumizi ya silaha na hivyo kunusuru maisha ya majambazi kwa upande mmoja lakini pia na kwa Polisi.
Kamanda Aziz amesema Polisi wamefanikiwa kuzima tukio hilo baada ya kuwa na taarifa za kutosha kutoka kwa wasiri wake ambao ni wananchi.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi, kwa kupitia falsafa ya Polisi Jamii, walipatie taarifa sahihi zitakazowezesha kukamatwa watuhumiwa waliotoroka nakuwataka watu wote wanaokwenda Benki kwa dhamira ya kuweka au kuchukuwa fedha nyingi wawe wasiri na kutoa taarifa Polisi ili wapatiwe usindikizaji salama wa fedha zao.

No comments:

Post a Comment