Thursday, January 3, 2013

Watuhumiwa watano wa ubakaji wa msichana wa miaka 23 wafikishwa Mahakamani nchini India na huenda wakahukumiwa kifo


Jeshi la Polisi nchini India hatimaye limewafungulia rasmi mashtaka watuhumiwa watano wa mauaji, utekajinyara na ubakaji wa msichana mwenye umri wa miaka 23 aliyekuwa anasomea Udaktari huko New Delhi.
Wanawake wa India wakifanya maandamano kushinikiza makundi ya wabakaji yachukuliwe hatua na kutokomezwa

Jeshi la Polisi limewasilisha ushahidi wake dhidi ya watuhumiwa hao watano wenye kurasa elfu moja ukieleza namna walivyotekeleza tukio la ubakaji ambalo limechangia kifo cha msichana huyo aliyepata majeraha makubwa.

Watuhimiwa hao watano wenye umri kati ya miaka 19 na 35 huenda wakakabiliwa na adhabu ya kifo kama wakikutwa na hatia ya kutenda kosa hilo dhidi ya msichana huyo aliyefikwa na umauti siku ya jumamosi.

Watuhumiwa hao watano hawakuwepo mahakamani wakati ushahidi huo unawakilishwa mbele ya Jaji anayesikiliza kesi hiyo kwa ajili ya kuanzwa kusikilizwa huku shinikizo kubwa likiendelea kutolewa ambapo wengi wanataka wakabiliwe na adhabu ya kifo.

Msemaji wa Polisi nchini India Rajan Bhagat amesema Jeshi liliwakamata watu sita likiwahusisha na tukio hilo la ubakaji wa msichana huyo tukio lililotokea kwenye basi la kubeba wanafunzi huko New Delhi.

Mwanasheria Mkuu wa India Altamas Kabir naye amejitokeza na kusema suala hili linastahili kuendeshwa kwa utaratibu wa hali ya juu ili kuepukana na makosa ya kisheria ambayo yanaweza yakijitokeza.

Kabir ametaka sekta ya sheria kutojisahau na kukiuka mipaka yao ya kuwatambua watu wakosaji hadi pale ambapo watathibitika wamekutwa na hatia kutokana na ushahidi uliopatikana na badala ya watu kusukumwa na hisia.

Jeshi la Polisi limelazimika kupendekeza adhabu ya kifo kama watuhumiwa hao watano kama watakutwa na hatia kutokana na uwepo wa maandamano ambayo yanataka adhabu ya wabakaji ibadilishwe.

Jiji la New Delhi limeendelea kushuhudia maandamano ya wanaharakati na wanawaka kila uchao ambao wamekuwa wakishinikiza serikali kuhakikisha inawalinda wanawake sambamba na kuyashughulikia magenge ya wabakaji.

No comments:

Post a Comment