Monday, June 3, 2013

Vuai apeleka mashambulizi kwa Maalim Seif kufanya usaliti wa kisiasa

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar 
Vuai Ali Vuai
Chama cha Mapinduzi Zanzibar kimemtaka Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad kuacha kufanya usaliti wa kisiasa na kuwasemea Wazanzibari kuhusu suala zima la mchakato wa Katiba, likiwemo suala la Muungano. 

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za CCM mjini Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Vuai Ali Vuai amesema hakuna kikao rasmi kilichofanyika na kufikia makubaliano ya kuwasemea Wazanzibari katika suala la Muungano. 

Vuai amesema CCM haitambui kamati ya maridhiano na kusisitiza kwamba Marais wastaafu Aman Abeid Karume na Dakta Salmin Amour bado ni watiifu kwa chama na kamwe hawawezi kwenda kinyume na sera za chama hicho katika masuala ya Muungano. 

Vuai ameshangazwa na kauli ya Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais kwa kumkosoa hadharani Rais Ali Mohammed Shein na badala yake kumpamba rais mstaafu Aman Abeid Karume. 

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar amesema, lengo la kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa lilikuwa ni kumaliza chuki za kisiasa, kuimarisha misingi ya amani na umoja wa kitaifa ili wananchi wa Zanzibar waishi kwa utulivu na amani.

No comments:

Post a Comment