Waziri wa Nishati na Madini, William Mganga Ngeleja (wa pili kushoto), akimkabidhi fulana ya CCM, aliyekuwa Katibu wa Chadema Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Stansilaus Manyanza, baada ya kukihama chama hicho na kujiunga rasmi na CCM leo.

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mwanza, kimeendelea kukitesa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya viongozi wapatao 30 wa ngazi ya Wilaya katika Wilaya ya Magu na Kwimba kurudisha kadi zao kisha kujionga na CCM.
Kwa ujumla wao, viongozi na wanachama hao wa Chadema, wamejiunga rasmi na CCM hii leo, baada ya kurudisha kadi zao na kukabidhiwa za CCM pamoja na fulana za chama hicho tawala, katika mkutano maalumu wa kuwapokea, uliofanyika katika ukumbi wa jengo la Nyanza jijini hapa.
Mwandishi wa mtandao huu kutoka jijini Mwanza, Sitta Tumma anaripoti kwamba; Mkutano huo ulioongozwa na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina na kuhudhuriwa na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Sengerema, Mathew Lubongeja, ulikuwa na ajenda moja tu ya kupokea wanachama hao wapya.
Mbali na mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Mwanza, Mabina kupokea kadi za wanachama na kuwakabidhi kadi za CCM, baadhi yao wanadaiwa ni wanachama hai wa CCM, lakini wamenunua kadi za Chadema na kujipajika nafasi ambazo si zao ndani ya Chadema ili kuuhadaa umma.
Miongoni mwa viongozi waliokuwa wa Chadema, ambao wamerudisha kadi na kutangaza rasmi kujiunga na CCM ni pamoja na aliyekuwa Katibu wa Chadema wilaya ya Magu, Stansilaus Manyanza pamojaDominic Manembe ambaye alidai ni kiongozi wa Chadema wilaya ya Kwimba.
Hili ni tukio la pili kwa viongozi wa Chadema kuhamia CCM, baada ya Januari 3 mwaka huu viongozi wa ngazi zote za wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza kutangaza kwenye mkutano wa hadhara kukihama chama hicho na kujiunga na chama tawala, mbele ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Wakizungumza kwenye mkutano huo maalumu wa kupokelewa ndani ya CCM, wanachama hao walikibeza waziwazi chama cha Chadema na sera zake, kwa kusema chama hicho kinaendeshwa kama familia ya mtu mmoja, huku wakimtaja Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibroad Peter Slaa kuwa ni 'mzinzi', na ndiyo maana alishindwa kwenye uchaguzi mkuu 2010 ngazi ya Urais.
Walisema, wameamua kuondoka ndani ya Chadema na kujiunga na CCM baada ya kubaini pumba na mchele, na kwamba, sera, taratibu na kanuni za chama tawala ni nzuri kuliko zile za upinzani, hivyo kuahidi kushirikiana vema na viongozi wa ngazi zote ndani ya CCM kwa ajili ya kujenga nchi.
Hata hivyo, aliyekuwa Katibu wa Chadema wilaya ya Magu, Manyanza alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi sababu hasa za kuondoka Chadema na kujinga na CCM alisema kwa kifupi kwamba: "Aisee, haya ni maisha tu...lakini Chadema Mwanza imeharibiwa na Katibu Wilson Mushumbusi".
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini, Ngeleja aliwapongeza wanachama hao wapya, na kusema kwamba moto uliowashwa Sengerema kwa viongozi wa Chadema kuhamia CCM utasambaa wilaya zote za mkoa wa Mwanza na taifa kwa ujumla, na hiyo inatokana na sera za CCM kuwa nzuri na madhubuti.
"Nawapongezeni sana wanachama wetu wapya tufanye kazi ndani ya CCM. Na hapa nasema moto niliouwasha Sengerema utasambaa wilaya zote za mkoa wa Mwanza. Utawaka hadi taifa zima, maana CCM haina mpinzani kwa sera nzuri na mwelekeo thabiti wa maendeleo ya wananchi", alitamba Waziri Ngeleja.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza, Mabina naye aliwamwagia sifa kemkemu wanachama hao wapya, na kuwaomba kushirikiana na viongozi wa chama hicho tawala kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Alipoulizwa na gazeti hili kuhusu tetesi za CCM kuanza kununua wanachama na baadhi ya viongozi wa Chadema mkoani hapa, Mabina alisema: "Tetesi hizo si za kweli, maana viongozi hawa wanakuja kwa matakwa yao wenyewe. Chadema haina nguvu ya kutubabaisha sisi CCM na kama wanabisha wasubiri 2015 hakuna hata mmoja wa Chadema atakayerudi kwenye uongozi".
Hata hivyo, Mabina alikiri wazi chama chake kuteleza na kupoteza baadhi ya majimbo na kata nyingi mkoani Mwanza, na kusema kwa sasa chama chake kimejipanga vizuri kuhakikisha kinanyakua majimbo na kata zote za mkoani hapa katika Uchaguzi mkuu ujao 2015.
Pia alikanusha kuwepo kwa taarifa za kufanya mazungumzo na mmoja wa wabunge wa Chadema mkoa wa Mwanza, kwa madai kwamba hawana utaratibu wa kununua viongozi, bali wanachama hao wanajiunga na CCM kwa hiari yao, na kama kuna mbunge anataka kuhamia CCM milango ipo wazi atapokelewa.