Friday, February 10, 2012

Uvujaji mitihani Tanzania: Zanzibar wanafutiwa matokeo; Bara wanarudia?

Katika kuthibitisha kuwa wanafunzi wa kizanzibari walikuwa wakikandamizwa na bado wanakandamizwa katika masuala ya mitihani inayosimamiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni haya yaliyotokea mwaka huu. Ni jambo la kawaida kutokea kesi za udanganyifu katika ufanyaji, na usimamizi wa mitihani ya taifa jambo ambalo huchukuliwa kama ni la kwenda kinyume na maadili na kanuni za mitihani hivyo. Linapotokea suala hili, baraza la mitihani la Taifa huwachukulia hatua wale wote waliohusika. Jambo hili si geni linaonekana kila mwaka pale baadhi ya wanafunzi kufutiwa matokeo na walimu kuchukuliwa hatua za kinidhamu ili kurejesha heshima na nidhamu ya mitihani.

Hata hivyo inapobainika kuwa usambazaji, ulinzi na usimamizi wa mitihani nao ulikuwa na matatizo na hivyo kuwa miongoni mwa sababu za kuharibika kwa mitihani hiyo, baraza la mitihani huwachukulia hatua wale waliosababisha kuvuja kwa mitihani na mitihani hiyo kurejewa upya. Hatua kama hii imeshawahi kuchukuliwa kwa baadhi ya mikoa kama Dar es Salaam na mengineyo kulazimika kurejea mitihani kwa kuwa mikoa hiyo imegundulika kuvujiwa na mitihani hiyo. Halkadhalika hatua kama hiyo imeshawahi kuchukuliwa kwa Tanzania nzima katika mwaka wa 1998 kwa kurejewa upya mitihani ya kidato cha 4.

Jambo kama hilo tulilitegemea pia kutokea kwa upande wa Zanzibar ambapo inaonekana mitihani ya kidato cha 4 ya mwaka 2011 inaonekana kukabiliwa na suala kama hilo. Hii ipo wazi kwani udanganyifu katika mitihani miaka yote hikuwahi kuwa wa kiwango na wa hali kama ilivyojitokeza mwaka huu. Hivi ni kweli hata wanafunzi wangu 15 wa kidato cha 4 wa skuli yangu ambao nawaamini hata kupata daraja la kwanza nao hawakujua kitu katika mitihani hiyo? na hivyo kulazimika kukopia majibu kutoka kwa wenzao katika vyumba vya kufanyia mitihani? Hivi inaingia akilini wanafunzi wote wa skuli husika wasweze kujiamini kufanya mitihani yao na kufanya vitendo vya udanganyifu katika vyumba vya mitihani? Hivi basi inawezekanaje skuli zaidi ya 7 zilizofutiwa matokeo ziwe na wanafunzi watupu wasio na uwezo wa kufanya mitihani bila ya kukopi majibu kwa wenzao? Tusisingizie udanganyifu wa wanafunzi tu, bali na mengine ya msingi yaliyosababisha tuyaseme. Tuwe wawazi, ukweli ni kwamba baadhi ya mitihani imevuja kabla ya kufanywa jambo lililopelekea wanafunzi kujadili kwa pamoja majibu na hivyo kufanana kwa majibu yao sahihi na yasio sahihi katika mitihani hiyo. Kwa mujibu wa kanuni za usahihishaji za NECTA kujitokeza kwa hali hiyo inatosha kuwa ni ushahidi wa kufanya udanganyifu.

Mimi sisitetei kuwa wanafunzi hawakudanganya, la hasha! ambacho ninahoji ni kwa nini wahukumiwe wanafunzi wakati wao walipotezwa na mitihani iliyovuja wakati wakiwa katika hofu ya mitihani? Ni kawaida mwanafunzi akiona maswali aliyopewa leo na kuwambiwa ni mvujo ameyakuta kweli katika mtihani, basi ni dhahiri  hatoacha kujadili na wenzake maswali mengine atakayopewa kwa kuamini ndio atafanikiwa katika mitihani. Huu ndio msingi wa tatizo ulivyo.

Nilipokwenda mimi, Katibu Mkuu wa Vijana Taifa Mhe. Khalifa Abdala Ali kama Uongozi wa vijana wa CUF Taifa pamoja na mwakilishi wa viti Maalum na Naibu Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi wa CUF Mhe. Bi Zakia ili kujua sababu ya tatizo hili na kuuuliza kama Serikali ya Zanzibar imeshafuatilia, akiwa ofisini kwake Mazizini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Abdalla Mzee (Mpangile) alijibu kuwa yaliyotendeka dhidi ya wanafunzi wetu ni haki na wao wanajiandaa kuwachukulia hatua zaidi za kinidhamu wasimamizi wa mitihani na walimu wote waliohusika na kusababisha hayo yaliyotokea. Tulipomhoji kuwa haoni kama hili jambo si la kawaida bali msingi wa tatizo ni la kuvuja mitihani, alijibu hata iweje wao kama wizara hawatauunga mkono udanganyifu kwa kuwa umetendeka kweli na NECTA imewaletea ushahidi bali watakubaliana na maamuzi ya NECTA ya kuwafutia matokeo wanafunzi akiwemo mototo wake mwenyewe aliyefanya mtihani yake katika skuli ya Laureate Internaional ya Zanzibar, skuli ambayo imefutiwa matokeo yake yote na kubakishwa matokeo ya wanafunzi watatu tu. Bwana Mpangile aliendelea kutupa maelezo kwa kutwambia kuwa watu kila jambo wanakimbilia kusema ni tatizo la muungano lna jambo hili pia watadai hivyo lakini sio kweli hili ni tatizo la wanafunzi wetu na walimu wetu.

Hata hivyo mimi binafsi na ujumbe tuliokwenda kwake hatukubaliani na hoja na misimamo ya Naibu Katibu Mkuu huyo kwani habari za kuvuja kwa mitihani zilipatikana lakini tukashangazwa na kuendelea kwa mitihani hiyo. Sasa tutegemee nini? Mi mwanafunzi yupi atakaepata jawabu sahihi na swali lake akalikuta katika mtihani asiliandike vilevile alivyolipata na kuliweka kichwani? Tuwe wawazi tatizo ni uvujaji wa mitihani uliodharauliwa kwa kuwa umeathiri zaidi Zanzibar, tusiwaonee wanafunzi. Njia pekee ni maitihani kurejewa upya kama ilivyo kawaida. Hili ni tatizo la pande mbili, NECTA ilizembea na kusababisha kuvuja kwa mitihani kwa upande mmoja na wanafunzi walikwenda na majibu yao katika chumba cha kufanyia mtihani kwa upande wa pili.

Wizara ya Elimu Zanzibar haitatenda haki kwa kukubali kufutiwa matokeo yao wanafunzi wengi kama ilivyotokea. Tunaiomba wizara iwache mzaha na siasa za kuabudu muungano, wahakikishe mitihani hii inarejewa si hivyo sisi kama viongozi wa vijana tutahamasisha maandamano Zanzibar nzima mpaka kieleweke kwani tunafahamu kuwa jambo kama hili likitokea kwa Tanzania bara mitihani hufanywa upya..



Source: http://www.wavuti.com/#ixzz1m0BJ5lCj

No comments:

Post a Comment