Thursday, March 22, 2012

Maalim Seif: Tulitikiswa, tumekuwa imara zaidi

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, jana alikabidhiwa taarifa rasmi juu ya mtafaruku uliojitokeza ndani ya chama hicho wakati yuko nje ya nchi kwa kipindi cha miaka mitano.

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema katika kipindi ambacho mwenyekiti huyo hakuwepo nchini, chama kilipata misukosuko ambayo kutokana na uimara wa viongozi wake , waliweza kukabiliana nayo na kuweza kupata ufumbuzi.
“Tulipata bughudha bughudha, lakini chini ya uongozi wa Makamu Mwenyekiti, tulifanikiwa kuziondoa. Chama kiko imara tangu ulipotuacha na huenda kimekuwa imara zaidi. Ushuhuda wa uimara huo ni mapokezi uliyopata wakati umati wa wananchi ulipokupokea uwanja wa ndege. Chama kiko ngangari kinoma,” alisema Maalim Seif.
Hivi karibuni Baraza Kuu la Uongozi la Taifa katika kikao chake kilichokuwa Zanzibar kilimtimua uanachama Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, na wenzake kadhaa kwa madai ya kuwa vinara wa uchochezi ndani ya chama.
Akifungua kikao hicho cha siku mbili cha Baraza la Uongozi, Profesa Lipumba, alisema yaliyotokea wakati hayupo yalikuwa madogo yakilinganishwa na yale ya mwaka 2001 wakati wakidai Katiba mpya, utawala bora, tume huru ambayo yalisababisha wenzao kadhaa kufariki na wengine kuwa wakimbizi, lakini serikali ilitii amri.
Kuhusu hali ya nchi, Profesa Lipumba alisema bado wananchi wake ni maskini, umaskini unaosababishwa na ombwe la uongozi uliopo madarakani.
Alisema njia pekee ya kuepukana na matatizo yanayoikumba nchi ni wananchi kukubali kufanya mabadiliko yatakayosaidia kuondoa hilo ombwe la uongozi.
Kuhusu rasilimali za nchi, alisema zipo nchi zilizopiga hatua kubwa ya maendeleo kutokana na viongozi walioko madarakani kukubali wananchi kumiliki rasilimali zilizopo.
Alisema kwa Tanzania umaskini unaweza kutoweka endapo tu utaratibu wa wananchi kumiliki rasilimali zao utaingizwa kwenye Katiba na kuwa wa kisheria zaidi.
Alitoa mfano wa rasilimali za madini, gesi na nyingine nyingi zilizo nchini ambazo alidai kuwa Watanzania hawafaidiki nazo na badala yake watu wachache na hasa wageni ndiyo wanaofaidika.
Profesa Lipumba alijigamba kuwa CUF ikiwa madarakani hayo yote yanawezekana na kuwataka wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama hicho kulipigia debe sana suala hilo ili wananchi waweze kuelewa kuwa CUF ni chama kinachojali maslahi ya makabwela.
Kuhusu matatizo ya umeme yaliyoikumba nchi sasa, alisema serikali iliwekeza sh trilioni 1.700 kwa ajili ya uzalishaji wa nishati hiyo, lakini cha kushangaza hali imezidi kuwa mbaya sana.
Alihoji fedha hizo zimepelekwa wapi na kama zimetumika, ni kwa ajili ya kazi gani ambayo imewanufaisha Watanzania.

No comments:

Post a Comment