Tuesday, September 18, 2012

Kutawazwa kwa Rais kwaashiria enzi mpya kwa Somalia


Rais wa Somalia aliyeondoka madarakani Sheikh Sharif Sheikh Ahmed alikabidhi rasmi madaraka kwa Hassan Sheikh Mohamud wakati wa sherehe za kutawazwa kwake katika Makao makuu ya Chuo cha Polisi huko Mogadishu Jumapili (tarehe 16 Septemba).

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud akizungumza wakati wa sherehe za kutawazwa kwake tarehe 16 Septemba jijini Mogadishu. [Mahmoud Mohamed/Sabahi]

Sherehe hizo, ambazo zilifanyika chini ya ulinzi mkali, zilihudhuriwa na watu wengi maarufu wa kimataifa na kikanda, wakiwemo rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh, Waziri Mkuu wa Ethiopia Haile Mariam Desalegn, Naibu waziri Mkuu wa Uturuki Bakir Bozdag na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Jean Ping.

Wawakilishi kutoka Uganda, Sudan, Qatar, Sudan ya Kusini, Iran, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Falme za Kiarabu na Asasi ya Ushirikiano wa Kiislamu pia walihudhuria sherehe hiyo.

"Leo, Somalia na Jumuiya za kimataifa zinashuhudia mtindo tofauti ambao haukuwahi kuonwa nchini Somalia kwa miongo minne, ambao ni kukabidhi madaraka kutoka kwa rais anayeondoka madarakani kwenda kwa rais aliyechaguliwa kidemokrasia," alisema mbunge, Mohamed Ahmed. "Hii ni mara ya pili katika historia ya Somalia kutokea kwa ukabidhianaji wa madaraka "

Kwa mara ya kwanza ilitokea miaka ya katikati ya 1960 wakati rais Aden Abdullahi Osman, Rais wa kwanza wa Somalia baada ya uhuru, kukabidhi madaraka kwa rais Abdirashid Ali Sharmarke.
"Hata hivyo kuna tofauti kati ya matukio haya mawili," Ahmed aliiambia Sabahi. "Leo furaha ni kubwa na yenye nguvu kuliko ile ya miaka ya miaka 1960 kwa sababu tukio tunalolishangilia leo limekuja wakati Somalia ikipitia mpito dhahiri wa kihistoria ambao utaitoa nchi kutoka kwenye serikali ya mpito kwenda kwenye serikali ya kudumu. Hatua hii itaonyesha enzi mpya katika historia ya Jamhuri mpya ya Somalia."

Ahmed Abdiqadir, mchambuzi wa masuala ya siasa anayeishi Mogadishu, aliwataka Wasomali kufanya kazi kwa dhati na uongozi mpya ili kuiondoa nchi katika matatizo ambayo imekuwa ikikabiliana nayo kwa miongo miwili iliyopita.

"Rais mpya hawezi kufanikisha kila kitu peke yake, ndiyo sababu Wasomali wote wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja na raisi mpya ili kuendelea mbele na kuijenga upya nchi," aliiambia Sabahi.

Abdiqadir alisema raisi mpya anapaswa kwanza kulenga katika ujenzi mpya na urekebishaji wa vikosi vyenye silaha ili viweze kufanya kazi ya ulinzi wa nchi. "Mwishowe, serikali mpya haitaweza kufanikisha utulivu katika nchi bila ya kuunda upya vikosi vya taifa," alisema.

Hussain Omar, mkaazi wa Mogadishu mwenye umri wa miaka 54, aliiambia Sabahi, "Wasomali wanamtarajia raisi mpya kuwa kiongozi mzalendo na kwamba ahadi zote alizotoa hazitaishia kuwa maneno matupu."

"Tunatumaini raisi mpya ataleta mabadiliko ambayo nchi hii inayahitaji sana. Nafikiri ni raisi ambaye anaelewa hali halisi ya nchi hii vizuri zaidi kwa sababu ameishi hapa kwa muda wa miongo miwili iliyopita wakati nchi ilipokuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe," alisema.

"Tunasali kwa ajili ya mabadiliko tunayoyataka na kwamba raisi mpya anaweza kuongoza nchi kuelekea katika amani, ustawi na ushindi."

Rais Mohamud aomba kutokomezwa kwa ugaidi na uharamia
Wakati wa hotuba yake ya kuapishwa, Rais Hassan Sheikh Mohamud aliahidi kufanya kazi ya kuimarisha ulinzi, kuiimarisha nchi kutokomeza ugaidi na uharamia nchini Somalia.

"Leo ni siku muhimu kwa wananchi wa Somalia," alisema. "Leo, tunafunga mlango na kufungua ukurasa mpya katika historia ya Somalia."

"Vipaumbele vyangu vya juu kabisa ambavyo ni vya kwanza, vya pili na vya tatu vitakuwa ni kuimarisha usalama na kurejesha utulivu kwa Somalia"

"Tunafanya kazi kuelekea kujenga jamii ambayo itaendelea kuwapo kwa amani pamoja na majirani na dunia kwa ujumla na tutafanya kazi kuelekea kuimarisha usalama wa nchi jirani badala ya kuunda serikali isiyofuata utaratibu na migogoro ya kutumia silaha," alisema.

"Sitakuwa tayari kuiongoza Somalia ya maharamia na magaidi," alisema Mohamud. "Tunataka Somalia iliyo huru dhidi ya uharamia na ugaidi na ninatumaini kwamba watu wa Somalia watakombolewa kutoka katika jambo lililokaririwa, ambalo wamekuwa wakijulikana dunia nzima: kwamba Somalia kuwa ni nchi ya ugaidi, Somalia kuwa ni nchi ya njaa, Somalia kuwa ni nchi ya uharamia."

Mohamud alirejelea mada ya upatanisho na majadiliano na Somaliland na kusisitiza umuhimu wa mazungumzo kama kipaumbele kimojawapo cha serikali yake.

"Nitashughulikia kuimarisha mapatano kati ya Wasomali na kuendelea na mazungumzo na utawala wa Somaliland kufanikisha umoja wa Somalia," alisema Mohamud. "Kufanikisha umoja wa watu wa Somalia kutatokea kupitia mazungumzo ya kujenga bila nguvu wala shuruti."

Alisema pia atafanya kazi ya kuendeleza uchumi wa nchi kwa kutoa ajira mpya, na kuahidi kuanzisha mfumo huru wa mahakama.

Rais aliyetoka madarakani Sheikh Sharif Sheikh Ahmed alisema, "Ni heshima yangu kubwa kuiona Somalia ikifikia hatua hii ya kihistoria [na] ninatoa wito kwa Wasomalia kufanya kazi na raisi mpya, serikali yake na bunge lake."

No comments:

Post a Comment