Thursday, December 29, 2011

Chadema: Ni hoja dhaifu kutuhusisha na Rashid

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekanusha vikali tuhuma za Chama cha Wananchi (CUF) dhidi ya chama hicho kuwa kinamtumia Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, kukivuruga chama hicho.

Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chadema, Erasto Tumbo, ameziita shutuma hizo kuwa ni hoja dhaifu isiyokuwa na msingi.
Akizingumza na NIPASHE jana, Tumbo alisema: “Sisi Chadema tutawezaje kuyafahamu mambo ya ndani ya CUF, kama kuna ukweli wowote tusubiri utajulikana.”
Aliongeza kuwa jambo muhimu kwa CUF ni kujitathmini na kumaliza zinazowakabili ndani ya chama chao badala ya kuhusisha na vyama vingine.
“CUF wanatakiwa warudi ndani ya chama na kuyatathmini matatizo yao,” alisema Tumbo.
Tumbo alisema CUF bila ya kuzungumzia mambo yao na kuvishutumu vyama vingine ikiwemo Chadema, watakuwa wanapoteza malengo yao kama chama cha siasa.
Baadhi ya viongozi ndani ya CUF wamekuwa wakidai kuwa Hamad Rashid ambaye amekuwa katika mvutano na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad, anatumiwa na Chadema na baadhi ya wanasiasa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mgogoro huo uliibuka hivi karibuni, baada ya Hamad Rashid kutaka Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais katika serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar, kuachia wadhifa wa ukatibu mkuu.
Kwa mujibu wa Hamad, kutokana na Maalim Seif kushikilia nafasi zote mbili, chama hicho kinaporomoka.

No comments:

Post a Comment