MAFURIKO YAONGEZA VIFO, MAJERUHI, MADARAJA,NYUMBA ZABOMOKA, BARABARA KUU ZAFUNGWA
Waandishi Wetu
WATU 11 wakiwamo watatu wa familia moja, wameripotiwa kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia mvua zilizoendelea kunyesha jana katika Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake na kuvuruga mfumo wa usafiri na shughuli za kiuchumi.Miondombinu mbalimbali ya Jiji hilo ikiwamo madaraja na nyumba vilivunjwa na kusababisha adha kubwa kwa wakazi ambao wengi wao, walishindwa hata kwenda kazini.
Baadhi ya barabara zikiwamo Morogoro eneo la Jangwani na Ali Hassan Mwinyi eneo la daraja la Salenda zilifungwa kwa muda kutokana na kujaa maji kiasi cha kuhatarisha maisha ya watumiaji wake.
Mvua hiyo ya siku mbili mfululizo kunyesha jijini Dar es Salaam, jana ilifanya maeneo mengi zikiwamo barabara muhimu kama Nyerere kuanzia Uwanja wa Ndege, Kawawa eneo la Kigogo Darajani na Mandela eneo la Tabata Matumbi, kushindwa kupitika kwa saa kadhaa kutokana na kujaa maji.
Katika barabara ya Mandela hali ilikuwa tete baada ya maelfu ya abiria waliokuwa wanasafiri kutoka Buguruni kwenda Ubungo, kukwama katika daraja la Matumbi.
Kwa zaidi ya saa nne tangu saa 1:00 asubuhi abiria walioonekana wakishuka kutoka kwenye magari na kutembea kwa miguu mithili ya maandamano, huku makumi ya magari yakiwa yamezimika barabarani.
Wakati hayo yakitokea, watumiaji wa barabara ya Mandela walikwama kutokana na msururu mrefu wa magari kufuatia baadhi yake kuzima na kufunga barabarani.
Katika barabara hiyo eneo la TIOT, ulionekana moshi mkubwa angani uliotokana na moshi wa gesi baada ya bomba linalopitisha gesi hiyo kupasuka. Moshi huo uliwafanya watu waliokuwa kwenye magari kupatwa na vikohozi.
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetaja mvua zilizonyesha jana na juzi kuwa hazijawahi kutokea katika miaka ya karibuni, na kwamba mara ya mwisho mvua kubwa kama hiyo ilirekodiwa mwaka 1954.
Madaraja yasombwa
Baadhi ya madaraja yalisombwa au kuvunjwa na maji hivyo kusababisha shida ya usafiri katika jiji hilo.
Daraja la Mbezi katika barabara ya Morogoro lililoko jirani na kibanda cha mkaa eneo la Tanesco lilivunika na kusababisha kukatika mawasiliano ya safari za kutoka na kwenda katikati ya jiji.
Mawasiliano katika daraja hilo yalikatika saa 11:00 alfajiri, na kusababisha misururu ya magari yaliyokuwa yakisubiri maji yapungue ili yapite.
"Hii leo sio kawaida, heri ya jana, sisi tumekwama tangu saa 10:30 alfajiri na mpaka sasa 1:45 asubuhi hatujui tutaondoka saa ngapi," alisema mmoja wa abiria waliokwama eneo hilo, ambaye alipiga simu ofisi za gazeti hili bila kutaja jina lake.
Vitus Andrew aliyejitambulisha kuwa ni dereva wa gari aina ya Mitsubishi fuso, alisema alifika eneo hilo saa 11.20 alfajiri na kukuta msururu wa magari ukiwa hautembei hivyo kumalazimu kuzima gari na kulala.
“Ndugu yangu, nimefika hapa mapema nikiwa naelekea Tabora, lakini naona safari yangu imeishia hapa kwa leo na kibaya zaidi hakuna kiongozi ama askari yeyote aliyefika kusimamia usalama wa abiria na magari kwani hali ya usalama si nzuri,” alisema Andrew.
Taarifa zilizopatikana baadaye, zilisema magari yalianza kupita kwenye daraja hilo saa 2:20 asubuhi.
Daraja la Mbezi Bondeni linalounganisha Mbezi Beach na Mwenge, wilayani Kinondoni limekatika upande mmoja kutokana na mafuriko hivyo kufanya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi cha Lugalo kuweka kambi maalumu kwa ajili ya kulinda usalama.
Hatua hiyo imesababisha wananchi wanaotoka Mbezi kuelekea Mwenge, kushindwa kutumia magari na kulazimika kuvuka kwa miguu kutokana na magari yote kuzuiwa kupita eneo hilo.
Daraja lililopo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lilijaa maji hivyo kulazimisha uongozi wa jeshi kuzuia magari yasipite kwa muda.
Maeneo mengine ya Jiji
Usalama wa maisha na mali kwa wananchi katika Bonde la Mto Msimbazi umekuwa hatarini kutokana na mvua hizo.
Mamia ya watu waliyakimbia makazi yao huku wengine wakiwa juu ya mapaa ya nyumba wakisubiri kuokolewa kutokana na nyumba zao kuzingirwa na maji.
Wengine walionekana juu ya minazi wakisubiri msaada kutoka kwa wasamaria wema huku helikopta ya polisi ikipita bila kuweza kutoa msaada wowote.
Mvua hizo zilisababisha balaa kwa wakazi wa eneo la Ubungo External, ambako maji ya Mto Ubungo yalisambaa kwenye makazi ya watu na kusomba mali zao.
Mwanamke ambaye ni mkazi wa eneo hilo ambaye jina lake halikufahamika mara moja, alisikika akisema tangu kuishi kwake Dar es Salaam miaka 34 iliyopita, hakuwahi kuona mafuriko ya aina hiyo.
Eneo la Mikocheni nako hali haikuwa shwari baada ya nyumba nyingi za wakazi wa eneo hilo kuzolewa na maji yaliyokuwa yanatokea katika bonde la mpunga, lenye mkondo wa maji ya bahari.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi walitaja sababu za eneo hilo kujaa maji kuwa ni ujenzi holela wa makazi ya watu hasa maeneo ya My Fair Plaza.
Amos John mkazi wa eneo hilo alisema umefika wakati Serikali ikachukua hatua za makusudi kuhakikisha mkondo huo wa maji unaachwa huru ili kunusuru maisha ya wakazi wa eneo hilo.
Katika eneo la Tandale kwa Tumbo, Mwananchi lilishuhudia watu wakiwa katika hali mbaya huku wakiomba msaada baada ya kuzidiwa na maji.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya nyumba kusombwa na maji, huku baadhi ya wamiliki wake wakionekana katika makundi wakiomba msaada.
Wakizungumza katika eneo hilo jana, walisema hali imezidi kuwa mbaya tofauti na juzi na kwamba sasa ndio wamepoteza mwelekeo wa maisha kabisa kwa kupoteza mali zao na vitu muhimu ambavyo wanavitegemea kwa ajili ya kuendesha maisha yao.
“Sio jambo jepesi kurudi katika hali ambayo nilikuwa nayo kwa sababu nimepoteza mali zangu zote hasa ukizingatia nilikuwa nafanya biashara. Vitu vilivyokuwa dukani kwangu vimechukuliwa na maji na sasa sijui wapi nitakimbilia kupata msaada,” alisema Salum.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa Kwa Tumbo, Zinduna Kimbonaga, alisema: “Hali siyo nzuri, kipindi hiki kunahitajika hatua za dharura ili kuwakomboa wakazi wa eneo hili”.
“Watu hawana makazi wala vyakula. Hali ni mbaya, Serikali inatakiwa kufanya jitihada za kutoa misaada ya chakula na malazi ili kuepusha magonjwa ya milipuko,” alisema
Kimbonaga ambaye pia alibainisha kuwa juzi, Mbunge wa Kinondoni Idd Azan, aliwapa misaada ambayo inahitajika kuongezwa.
Mbagala, Tabata Kimanga
Wakazi wa kata ya Kijichi, jana walilazimika kutembea kwa miguu hadi maeneo ya Mtongani na Misheni kutokana na kukatika ghafla kwa mawasaliano ya usafiri katika daraja la Kijichi.
Daraja hilo lilifurika maji na hivyo kufanya magari madogo zikiwamo Hiace kushindwa kupita eneo hilo na yale yaliyofanikiwa kupita yaliongeza nauli hadi Sh500 badala ya kati ya Sh300 na Sh400.
Daraja lililopo kati ya eneo la madukani na chama, lilifurika maji hivyo kufanya watu wanaoishi Tabata Kimanga kushindwa kwenda makazini.
Daraja hilo lilianza kufurika maji saa 12:00 asubuhi na kupungua saa 3:00 asubuhi ambapo magari yenye uwezo mkubwa kama Toyota Land Cruiser na Defender yalianza kupita.
Magari mengi ya abiria yalishindwa kuendelea na safari kutokana foleni pamoja na barabara nyingi kujaa maji.
Pia nyumba zilizopo katika bonde hilo zilifurika maji huku nyingine zikibomoka kabisa hali iliyofanya watu walioshindwa kuwahi kuyakimbia maji hayo, kupanda juu ya dari na kubaki kuchungilia nje jinsi mali zao zinavyosombwa na maji.
Hali hiyo pia ilijitokeza eneo la Tabata Msimbazi, ambako taharuki ilijitokeza baada ya maji ya mto Msimbazi kujaa kwenye nyumba za watu.
Maji hayo yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha kuanzia saa 10 alfajiri ya kuamkia jana na yalisababisha wakazi wa eneo la Msimbazi Nyaluhela na Kwa Swai, hususan wanawake na watoto kutimua mbio kwenda maeneo ya Mwinuko kwa ajili ya hifadhi.
Cosmas Ndijo kutoka eneo Tabata Bima kwenye mwinuko alisema aliona mto huo ukisomba mizoga ya ng’ombe, mbuzi, kondoo, meza, viti na magodoro.
Naye Baraka Bansy alisema Mto Msimbazi ulijaa maji mengi na kusomba miti mingi kutoka mbali na kwamba, nyumba nyingi eneo la Msimbazi zilikuwa zimezingirwa na maji.
“Maji yamefika msikiti wa Msimbazi, wanawake na watoto wanazidi kutimua mbio kuokoa maisha yao,” alisema Baraka.
Kadhalika mvua hiyo ya jana ilisababisha barabara ya Umoja kuanzia Bima kwenda kwa Msimbazi kujaa maji na kusababisha watu kuvua viatu kupita eneo hilo.
Usafiri wa daladala na teksi kutoka Tabata kwenda Buguruni ama Ubungo, ulisimama asubuhi ya jana kutokana na maji ya mto Msimbazi kupita juu ya daraja.
Matumbi huku eneo la Tabata Relini nalo likijaa maji ambayo yalisababisha kupasuka kwa bomba la gesi.
Mabomba ya gesi yalipasuka kwenye eneo la viwanda vilivyopo Kituo cha TOT barabara ya Mandela na kusababisha moshi uliojaa harufu mbaya ambayo ilisababisha watu wengi kufadhaika.
Vifo Kinondoni
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema maji yalikuwa yamejaa pia kwenye ofisi za Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Taifa (UNDP).
Kamanda Kenyela alifafanua kwamba juhudi za uokoaji zilikuwa zikiendelea kwa watu waliokuwa ndani ya ofisi hizo.
Habari kutoka katika Hospitali ya Mwananyamala zinasema, kulipokelewa maiti saba na majeruhi watano katika hosipitali hiyo.
Muuguzi wa zamu wa hospitali hiyo Marry Shayo aliliambia gazeti hili kuwa kati ya maiti hao watatu ni wa familia moja. aliwataja kuwa ni Tatu, Sharifa na Amran wote wa ukoo wa Abeid. Maiti wengine ni wanne hawajatambuliwa.
Shayo alitaja majeruhi kuwa ni Husna Rashid mkazi wa Kigogo, Amina Rashid, Yonas Maganga, Sharifa Said na Ally Mdowa.
Kwa upande wake, diwani wa Kata ya Tabata, Mtumwa Mohamed alisema ameshuhudia miili ya watu sita ikielea katika maji yaliyokuwa yanapita kwa kasi katika Mto Msimbazi eneo la Matumbi, Tabata jijini Dar es Salaam, jana.
"Wale ni marehemu, hiyo haina ubishi kwani hakuna hata mmoja ambaye alikuwa anajaribu kujitetea" alisema na kuongeza kuwa watu hao ni tofauti na wengine zaidi ya sita waliokuwa wamepanda juu ya mti aina ya mwarobaini ambao nao ulisombwa na maji na kudondoka nao," alisema na kuongeza:,
"Hali si nzuri nafikiri watu wengi zaidi watakuwa wamepoteza maisha. Pia kuna taarifa za mtu mwingine kuchukuliwa na maji baada ya kurudi nyumbani kwake kwenda kuwaokoa watoto wake."
Alisema mwanaume ambaye ni maarufu kwa jina la Bonge wa eneo la Matumbi, alitoka nje kwa madai kwamba anawafuata watoto wake na hakuweza hata kupiga hatua tatu akasombwa na maji.
"Nilifika pale muda mfupi baada ya tukio na kuelezwa kuwa kuna mtu kasombwa, alikuwa anairudia familia yake," alisema na kuongeza kuwa hali ni mbaya katika kata yake na watu wengi zaidi huenda wamepotza maisha.
Baadhi ya watu wamedai kuwa kundi la watu wanane ambao walishika mikono kuvuka katika eneo la Matumbi ambalo lilijaa maji, lilisombwa na maji wakati wakijaribu kuvuka hali ambayo iliwafanya vijana wa eneo hilo kuzuia mtu yeyote asijaribu kuvuka.
Katika eneo la Kigogo, watoto watano wa familia moja waliripotiwa kupotea na tayari baba yao Issa Rajabu Mkazi wa Kigogo, aliliambia gazeti hili kuwa watoto hao na mama yao, walipotea muda mfupi baada ya maji kujaa kwenye nyumba yao.
“Mpaka sasa hivi nimewapata watoto wawili, bado watatu sijui walipo,” alisema Rajabu.
Rugimbana
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na Kaimu Mkuu wa Wilaya za Ilala na Temeke, Jordan Rugimbana alisema watu wanne walifariki dunia katika tukio hilo katika wilaya ya Kinondoni.
Alisema kutokana na janga hilo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick ameagiza kuundwa vikosi kazi maalumu kwa ajili ya kuhakikisha wanatoa msaada kwa wananchi walioathirika hasa katika Bonde la Msimbazi ambalo lilionekana kuathirika sana.
Alisema vikosi kazi hivyo vitafanya kazi kutambua maeneo yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na Msalaba Mwekundu, kutenga maeneo maalumu ya kupokelea wananchi.
Alitaja maeneo hayo kuwa ni Shule ya Sekondari Kibasila katika Wilaya ya Temeke, Shule ya Msingi Kilimani Rutihinda (Kinondoni) na Msimbazi katika Manispaa ya Ilala.
Hosipitalini Muhimbili
Ofisa Uhusiano Msaidizi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Jeza Waziri alisema wamepokea majeruhi wawili na maiti moja.
Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Deo Joseph (24) kutoka Tandale na Ibrahim Batazani (30) anayetokea Ilala na kwamba walifikishwa hospitalini hapo saa 9.30 mchana.
“Tumepokea majeruhi wawili na wametambulika na maiti moja ya mwanamke ambayo hadi hivi sasa haijatambulika, hawa majeruhi wanafanyiwa uchunguzi haijajulikana kama watalazwa au wataruhusiwa,”alisema Waziri
Mbowe asitisha ziara
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amelazimika kukatisha ziara jimboni kwake Hai kutokana na maafa yaliyowapata wananchi wa Dares Salaam.
Mbowe alifafanua kwamba amelazimika kusitisha shughuli hizo jimboni na nyingine kitaifa katika kipindi hiki kigumu, ambacho taifa kimeingia.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni kiongozi wa Upinzani Bungeni, aliwapa pole wote walioguswa na maafa hayo kwa namna moja au nyingine, ikiwa ni pamoja na kupoteza mali na ndugu.
Zitto Kabwe atoa change moto
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amewapa pole watu wote wa Dar es Salaam kutokana na madhara ya mvua.
“Ninawapa pole watu wote wa Dar es Salaam, pia tujitokeze kwa wingi kusaidia Watanzania wenzetu waweze kurejea katika maisha ya kawaida. Pia kwa upande wa Serikali hii ni changamoto ya kuboresha mipango miji ya Jiji la Dar es Salaam,” alisema
Zitto alisema kwamba viongozi waache kukaa ofisini katika kipindi hiki na badala yake watembee makazi ya watu ambao wamepata maafa haya. “Nimepita maeneo mbalimbali, hali ya maisha ya hawa Watanzania wenzetu inatisha. Tushirikiane na tuwe wamoja kipindi hiki kigumu,” alisema
No comments:
Post a Comment