MBUNGE wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), amesema baadhi ya viongozi wa chama hicho wanauonea wivu urafiki wake na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na hivyo kuzusha uongo kuwa anamhonga fedha ili akidhoofishe.
Aidha, amesema, tofauti na inavyodaiwa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Julius Mtatiro kuwa anakibomoa, atakuwa mtu wa mwisho kufikiria kufanya usaliti huo kwa kuwa anakipenda na amechangia nguvu nyingi kukifikisha kilipo, ikiwemo hali na mali.
Alisema hayo jana alipozungumza na gazeti hili kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwake na Mtatiro, zikimhusisha na uchochezi wa vurugu zilizotokea katika Tawi la CUF la Chechnya, Mabibo jiini Dar es Salaam siku tatu zilizopita na kusababisha umwagaji wa damu.
“Mtatiro anazungumza mambo asiyokuwa na uhakika nayo. Anavuka mipaka kwa kumhusisha
Waziri Mkuu na kudhoofika kwa CUF huku akijua kuwa sio kweli.
Yeye na wenzake wanaotangaza kuwa nimehongwa na kiongozi huyo shilingi milioni 700 ili nikisambaratishe chama, wanasema uongo kwa lengo la kumchafua, ni rafiki yangu na wivu walionao juu ya urafiki wetu ndio unaowasumbua.
“Haikatazwi kuwa na rafiki kutoka serikalini na wala haijaelezwa mahali kuwa ukiwa karibu na
kiongozi, basi unatumiwa kukiharibia chama chako.
Huo ni wasiwasi wao tu unaotokana na fikra dhaifu kwa sababu nina uhuru wa kuwa na marafiki. Wamuache Pinda, hahusiki na matatizo ya CUF,” alisema mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa Waziri katika Serikali ya Muungano na pia Kiongozi wa Upinzani Bungeni.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mtatiro alisema Kamati ya Maadili na Nidhamu ya CUF itamwita Hamad na wenzake; Hassan Doyo, Yassin Mrotwa na mbunge wa zamani, Shoka Khamis Juma wakati wowote ili wajieleze juu ya utovu wa nidhamu na uchochezi wa vurugu uliosababisha kutokea kwa vurugu katika eneo hilo la Mabibo.
Kwa mujibu wa Mtatiro, haikuwa nia ya CUF kuanika mambo hayo hadharani, lakini kutokana
na kukithiri kwa vitendo vya kukichafua chama hicho vinavyofanywa na Hamad pamoja na wajumbe wenzake wa Baraza Kuu la Taifa, wameona ni lazima waujulishe umma juu ya kinachoendelea, ili uufahamu ukweli.
“Tukiendelea kunyamaza chama kitaharibiwa sifa na kusambaratishwa na ‘waasi’ hawa wanaohongwa fedha na kiongozi mmoja wa serikalini ili waiue CUF. Hamad ni kiongozi wa juu katika CUF, lakini haiheshimu wala kuifuata Katiba ya CUF, ana kazi ya kuchekacheka na Pinda tu,” alidai Mtatiro na kuongeza: “Anachochea vurugu na kutumia fedha kukiharibu chama kwa
kuhonga Sh 200, 000 kwa vigenge vya wahuni ili vihatarishe amani na kukichafua…nina ushahidi wa ninachokieleza”.
“Katiba imetoa mwongozo wa nini kifanyike kudhibiti watovu wa nidhamu kama yeye (Hamad)
kabla ya kuhatarisha zaidi amani ya wananchi. Alisababisha vurugu Mabibo juzi tu katika tawi la CUF la Chechnya na kuwafanya walinzi wetu wa chama wanne wakatwe mapanga.
Tumechukua hatua kwakufungua kesi ya shambulio la kudhuru mwili katika Kituo cha
Polisi Magomeni na hatua nyingine za kichama zinafuata.”
Alidai CUF imebaini sababu za Hamad na wenzake kufanya uchochezi huo ni kuwavunja moyo viongozi wenye nia njema na wanaozingatia Katiba kutekeleza majukumu yao, ikiwa ni pamoja na kukiimarisha.
“Sijui ni mapenzi gani aliyonayo Hamad kwa CUF kwa sababu anatenda tofauti na inavyoelekezwa na Katiba ya chama. Anafanya mikutano bila kufuata utaratibu na anapohojiwa na walinzi wa chama wanaofanya kazi kwa mujibu wa Katiba, anawapambanisha
na ‘wahuni’ wake na kufanya waumizwe kwa mapanga,” alidai.
Alitolea mfano vurugu za Mabibo, Dar es Salaam na kueleza kuwa zilifanywa na ‘watu wake’ zaidi ya 100 dhidi ya walinzi wa CUF wanane baada ya kupewa maelekezo na Hamad aliyekwenda katika eneo la tukio baadaye kwa madai ya kutuliza fujo.
Aidha, aliweka bayana kuwa pamoja na kuwakatisha tamaa ya kazi viongozi waliokuwepo
madarakani, Hamad anatumia njia hiyo isiyo sahihi kujitengenezea njia ya kuupata ukatibu mkuu wa CUF mwaka 2014.
“Ni jambo la kushangaza kwa sababu cheo hicho kitagombewa mwaka 2014 na yeye anaanza purukushani leo mwaka 2011, kuna nini au ana lingine la zaidi?
Na fedha anazozihonga kwenye matawi ya chama ili apate fursa ya mikutano isiyozingatia taratibu anazitoa wapi?” Alihoji Mtatiro.
Akijibu tuhuma hizo, Hamad alisema alikwenda katika tawi hilo kwa mwaliko maalumu wa maandishi na kwamba Sh 250,000 alizozitoa katika tawi, zilikuwa mchango wa tawi alioombwa na wahusika.
“Ni mkutano wa kikatiba wa tawi ambao hauhitaji kupata kibali wala kuutolea taarifa, Mtatiro
haelewi Katiba, mimi nilikuwa mwalikwa tu na nilitoa fedha hizo hadharani. Sikukiuka Katiba,”
alisema Hamad.
Kuhusu kuwania ukatibu mkuu, alisema sio siri kwa sababu alitangaza nia tu na wala hafanyi
kampeni.
“Naona Mtatiro ana wasiwasi sana na mimi, nilimwandikia Mwenyekiti wa Chama Taifa kuhusu nia yangu ya kugombea ukatibu mkuu na kutangaza nia hiyo katika maeneo mengine husika,
sasa hilo ndio lisababishe nikialikwa katika mikutano ya matawi nisiende?
Sioni kosa langu na wakiniita katika Kamati hiyo nitakwenda kuwasikiliza na kujibu hoja,” alisema Hamad na kukana kupanga wahuni kufanya vurugu.
No comments:
Post a Comment