Tuesday, December 13, 2011

Zitto amkingia kifua Nape

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), ameutaka umma usimbeze Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi, Nape Nnauye juu
ya tamko lake la kupinga posho mpya za wabunge kwa kusema alichofanya ni hekima za harakati.

Zitto ambaye ameeleza kusikitishwa na watu wanaombeza Nape, amesema katika siasa ya nchi kama Tanzania, busara ya mapambano ni jambo la msingi.

“Kama Nape wa CCM anaunga mkono hoja ya upinzani kuhusu posho, asibezwe wala kuzodolewa. Anapaswa kuungwa mkono ili kuongeza jeshi na kumkinga dhidi ya wapenda posho ndani ya chama chake,” alisema Zitto kupitia kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Alisema, “Hii ndio huitwa hekima za harakati. Nimesikitishwa sana na wanaobeza kauli ya Nape kuhusu posho za wabunge.”

Akiendelea kusisitiza Nape aungwe mkono, Zitto alisema, “Lengo letu haswa nini? Kwamba
Zitto aonekane mshindi? Hapana.

Kwamba Chadema ionekane mshindi? Hapana. Lengo letu ni kuondoa posho za vikao kwa
wabunge na viongozi wa umma.

Lengo letu ni mwananchi wa Tanzania ashinde kwa kupunguza matumizi mabovu. Ye yote anayeunga mkono lengo hilo tunapaswa kumwunga mkono”.

Zitto aliendelea kusema, “Nape awe kajisemea yeye au chama chake, haijalishi, muhimu posho
hizi ziondoke. Ukimbeza Nape leo, siku nyingine atashindwa kufanya alivyofanya sasa.

Mbaya zaidi wenzake huko kwenye chama chake watamchukia kwa uamuzi huu, huku nje nako mkimbeza mnapoteza mpiganaji.

“Hii inaitwa busara. Hatushindani hapa. Tunataka posho ziondoke. Nape anakubaliana nasi.
Aungwe mkono ili sauti yetu iwe kubwa zaidi”.

Wakati baadhi ya watu wanaelezea kubeza tamko hilo la CCM kuwa ni kujisafisha, Zitto
ameendelea kutetea kwa kusema, “kama wanajisafisha kwa kuunga mkono hoja yetu kuna ubaya gani?”

Alisema shinikizo likiwa kubwa kama ambavyo vyama vyote vikuu vya siasa vilivyotoa kauli kupinga posho hiyo mpya, itazuia malipo yake kuendelea.

Aliuasa umma usipoteze nguvu ya kupinga posho kwa kuanza kuangaliana kivyama, bali upinzani ufanyike bila kujali itikadi za kisiasa.

Alisema jambo la muhimu ni kuhakikisha juhudi zinafanyika ili wabunge wengi wa CCM wakubali hoja ya kupinga posho hizo.

“Ndiyo maana nasema tusimbeze Nape, tumwunge mkono. Ni muhimu katika kampeni yetu ya
kuondoa posho za vikao,” alisema Zitto.

Katika mijadala mbalimbali isiyo rasmi inayoendelea ama kwenye mitandao ya kijamii au
mazungumzo, kumekuwepo na maswali juu ya ni nani mwenye uamuzi wa kusitisha posho hizo
iwapo chama tawala ambacho Mwenyekiti wake ni Rais Jakaya Kikwete pia kinalalamika.

Hata hivyo, Chadema kupitia kwa Zitto kinaelezea kufurahishwa na kuwepo mgawanyiko wa kimawazo ndani ya CCM juu ya posho kwa kusema kitendo cha Nape kupingana na Spika wa
Bunge, Anne Makinda ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu, ni ushindi kwa Chadema kinachokataa fedha za umma kutapanywa hovyo.

Wiki iliyopita, CCM kupitia kwa Nape ilitoa tamko la kupinga ongezeko la posho za wabunge
kwa takribani asilimia 200 kutoka Sh 70,000 hadi Sh 200,000.

Ilisema kwa kuongeza kiwango hicho cha posho ni kuongeza tofauti ya mapato kati ya wenye nacho na wasionacho.

Nape alishauri busara itumike kuachana na jambo hilo kwa kuwa kuendelea nalo kunaweza kutafsiriwa kuwa ni kuwasaliti watendaji katika sekta nyingine wakiwemo walimu, askari, madaktari na wengineo.

Wakati huo huo, Zitto amesema kwamba taarifa alizonazo ni kwamba Rais Jakaya Kikwete
hakupelekewa maombi ya kutakiwa apitishe nyongeza ya posho na kusisitiza kuwa hadi sasa hajasaini.

Kwa mujibu wa Zitto, vyanzo vyake vya uhakika vya habari vinasema kwamba Spika hakupeleka maombi yoyote kwa Rais kwa ajili ya nyongeza hizo.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, aliwasiliana na mmoja wa watumishi katika Tume ya Huduma za
Bunge na kuambiwa kwamba posho ya vikao lazima iguse watumishi wote wa umma kwa maana kama kuna ongezeko lolote lazima liguse watumishi wote.

Aidha, amesema kwamba posho zinapaswa kufutwa na badala yake, nchi inapaswa kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Alisema inatubidi kufanya kazi na kuweka mazingira mazuri kwa shughuli za kiuchumi ambazo zinatengeneza ajira, zinaongeza thamani ya uzalishaji wake, kuongeza usafirishaji bidhaa nje, kuzalisha chakula zaidi na

No comments:

Post a Comment