Monday, December 12, 2011

Maalim Seif, Hamad Rashid waingia vitani

Msuguano baina ya viongozi waandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF), Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, lakini jana ilithibitika kuwa ni kweli baada ya ziara ya kutembelea matawi na kugawa vifaa kuvurugwa na walinzi wa chama (Blue Guards) kutoka makao makuu.
Ziara hiyo ilikuwa inafanywa na Hamad Rashid katika kata ya Manzense, lakini alipofika kwenye tawi la Kosovo, walinzi hao walilivamia wakieleza kuwa hakuna shughuli inayoruhusiwa kwenye eneo hilo kwa kile kilichodaiwa kuwa makao makuu ya chama Buguruni hayakuwa na taarifa wala baraka za ziara hiyo.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa Hamad Rashid alifika kwenye shina la Kosovo majira ya saa 3:30 akapokewa na baadhi ya wanachama ambao walimwongoza kwenda ofisi za kata ya Manzese za CUF.
Habari zinasema kuwa Mbunge huyo alipokewa na viongozi wa kata wa CUF na kuzungumza nao kuwa alikuwa amefika kukabidhi vifaa vya ofisi. Alikabidhi viti na meza.
Akizungumza na wanachama hao baada ya kukabishi vifaa hivyo, Hamad Rashid alisema kuwa wakati sasa umefika wa kufanya mabadiliko ya katiba ya chama ili kiende na mabadiliko ya sasa kwa sababu anaona kuwa kinapoteza mvuto wa kisiasa mbele ya wananchi.
BLUE GUARDS WAVAMIA
Hamad Rashid akiwa bado anazungumza, walifika Blue Guards na kuzingira eneo hilo kisha wakaingilia mkutano huo, na kumtaka aache kuzungumza na aondoke.
Baada ya tukio hilo, Hamad Rashid aliondoka eneo hilo na kuacha mzozo baina ya wanachama wa CUF juu ya ziara hiyo.
Katika mzozo huo, Blue Guards walisema kuwa Hamad Rashid alikuwa amekiuka utaratibu wa chama kwa kufika ofisi za mashina na kata bila wilaya, mkoa na makao makuu kuwa na taarifa za ziara yake kwa kuwa si sehemu ya jimbo lake.
Hata hivyo, baadhi ya wanachama waliokuwa eneo hilo waliunga mkono kauli ya Hamad Rashid kuwa kuna haja ya kufanyika kwa marekebisho ya katiba ili iwe na mvuto zaidi.
Vyanzo vya habari zaidi viliiambia NIPASHE kuwa magari mawili yaliyojaa walinzi wa chama hicho yaliondoka Buguruni kwenda Manzese kwa maagizo ya viongozi wa makao makuu ya kuzuia ziara ya Hamad Rashid ambayo inatafsiriwa kama ya kujijenga kisiasa Tanzania Bara ambako amekuwa akimtuhumu Katibu Mkuu Maalim Seif kuwa ameshindwa kukijenga chama upande huu wa Muungano.
MTATIRO ATOA TAMKO
Akizungumza na NIPASHE kuhusiana na tukio hilo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro, alisema kwamba makao makuu ya chama taifa, haikuwa na taarifa ya ziara hiyo kama ulivyo utaratibu wa chama.
“Unajua sisi CUF, tuna utaratibu wa ziara za viongozi wetu waandamizi ndani ya chama, yaani wabunge, wawakilishi, wajumbe wa baraza kuu na kwamba wanapofanya ziara yoyote iliyo nje ya maeneo yao, hupaswa watoe taarifa kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu. Utaratibu huu, hata mheshimiwa Rashid anaufahamu. Ofisi ya Katibu Mkuu haikuwa na taarifa ya ziara hiyo,” alisema.
Akizungumza pendekezo la Hamad Rashid la kubadili katiba ya chama, Mtatiro alisema kwamba chama hicho kina utaratibu kwa mwanachama wake mwenye nia, maoni au mapendekezo ya kubadili katiba ya chama na siyo kutumia njia za “panya” kwa kuwa hazitafanikiwa.
Mtatiro alisema kwamba masuala yote yanayohusu chama hicho huamuliwa na vikao vya chama ambavyo ni Baraza Kuu na Mkutano Mkuu na hivyo akashauri wanachama wote wenye jambo lolote kulipitisha katika vikao vya chama.
“Huwezi ukabadili katiba ya chama kwenye vijiwe au Manzese, kama mwanachama ana mchango au mbinu anayodhani inaweza ikatusaidia ailete na ndivyo utaratibu ulivyo na ndivyo kazi zinavyofanyika,” alisema.
Ingawa Mtatiro hakuwa tayari kueleza alivyojua kuwa Hamad Rashid alikuwa Manzese, kuwasili kwa walinzi wa makao makuu kwa ajili ya kuvuruga au kuvunja ziara yake ni kielelezo kingine juu ya malalamiko ya Mbunge huyo kuwa Ofisi ya Katibu Mkuu wa CUF inamuhujumu kisiasa.
Hamad Rashid amekwisha kuwasilisha malalamiko kwa Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, juu ya vitendo vya ‘hujuma za kisiasa’ vinavyofanywa dhidi yake ama kwa baraka za Maalim Seif au kwa maamuzi yake binafsi.
Juhudi za kumpata Katibu Mkuu wa CUF Taifa, Maalim Seif kwa njia simu jana kuzungumzia suala hilo zilishindikana.
CHIMBUKO LA UHASAMA
Chimbuko la hali hii linadaiwa ni vuguvugu za ndani kwa ndani za uchaguzi wa viongozi wa chama hicho akidaiwa kutamani kiti cha Katibu Mkuu kitakaachoachwa wazi na Maalim Seif kama ataamua kustaafu.
Hamad Rashid analalamika kuwa Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, ana mwanachama anayemuandaa kwa ajili ya kiti hicho.
Harakati hizo pia zimesababisha viongozi hao wawili kulaumiana juu ya utendaji na ujenzi wa chama Tanzania Bara, huku Hamad Rashid akimlaumu Maalim Seif kwa kutokufanya kazi kubwa ya kisiasa Tanzania Bara.
Miongoni mwa lawama anazobebeshwa Maalim Seif ni kufanya vibaya kwa CUF katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, ambao chama hicho kilishika nafasi ya tatu huku kikipata idadi ndogo ya wabunge Bara kiasi cha kupoteza nafasi ya kuunda kambi rasmi ya upinzani bungeni nafasi ambayo wameishikilia tangu mwaka 1995.

No comments:

Post a Comment