TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati ya Utendaji ya Taifa ya Chama Cha Wananchi (CUF) imefanya kikao chake cha kawaida cha siku mbili mjini Zanzibar tarehe 30 – 31 Desemba, 2011 chini ya Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Sharif Hamad.
Pamoja na kujadili ajenda kadhaa za kawaida kuhusiana na mambo ya utendaji katika Chama, Kamati ya Utendaji ya Taifa pia ilipata nafasi ya kupokea taarifa ya kina kuhusu hali ya kisiasa ndani ya Chama kutoka kwenye Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Chama kupitia Kamati yake Ndogo ya Nidhamu na Maadili. Taarifa hiyo ilijikita zaidi katika njama zinazoendeshwa na wanachama 14 wakiongozwa na Mheshimiwa Hamad Rashid Mohamed zenye mwelekeo wa kutaka kukivuruga Chama.
Kamati ya Utendaji ya Taifa imeridhika kwamba kuna hoja za msingi na ushahidi wa kutosha dhidi ya wanachama hao 14 unaoonesha kuhusika kwao na njama hizo. Wanachama hao ni:
1. Hamad Rashid Mohamed2. Doyo Hassan Doyo
3. Shoka Khamis Juma
4. Juma Said Saanani
5. Yasin Mrotwa
6. Mohamed Albadawi
7. Mohamed Masaga
8. Doni Waziri
9. Yusuf Mungiro
10. Nanjase
11. Ahmed Issa
12. Tamim Omar
13. Amir Kirungi
14. Ayubu Kimangale
Kwa mujibu wa Katiba ya Chama, kifungu cha 63 kinachozungumzia Wajibu wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, kifungu cha 63 (1) (d) kinafafanua wajibu huo kuwa ni “kulinda na kuendeleza heshima ya Chama na Serikali zote halali za nchi.” Kifungu cha 63 (1) (j) kinaelezea wajibu mwengine kuwa ni “kuwachukulia hatua za nidhamu viongozi na wanachama wanaoshutumiwa kwa makosa mbali mbali kwa kufuata masharti ya Katiba hii na kanuni zitakazotungwa mara kwa mara kwa mujibu wa katiba hii.”
Kwa kuzingatia hali hiyo, Kamati ya Utendaji ya Taifa imeridhika kwamba kuna haja ya kutumia uwezo iliopewa chini ya kifungu cha 62 (1) cha Katiba ya Chama kuitisha kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama ili kutafakari hali hiyo, kusikiliza tuhuma zinazowakabili wanachama hao, kuwapa nafasi ya kuwasiliza na kujitetea na kisha kuchukua hatua kama litakavyoona inafaa.
Kikao hicho cha Baraza kuu la Uongozi la Taifa kitafanyika Zanzibar, tarehe 04/01/2012 katika ukumbi wa hoteli ya Mazson.
Kamati ya Utendaji ya Taifa inawaomba wanachama na wapenzi wote wa CUF kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki na kutoa nafasi kwa vikao vya Chama kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Katiba ya Chama.
HAKI SAWA KWA WOTE
Imetolewa na;
JULIUS MTATIRO,
NAIBU KATIBU MKUU (TANZANIA BARA),
KATIBU WA KAMATI YA UTENDAJI TA TAIFA (CUF NATIONAL CENTRAL COMMITTEE).
31 Disemba 2011,
ZANZIBAR.
Saturday, December 31, 2011
Maamuzi ya kamati ya utendaji ya CUF - Taifa (kikao kimemalizika leo Zanzibar)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment