Sunday, January 1, 2012

JK aonywa





















ASEMA ATAUNDA TUME YA KATIBA NDANI YA MIEZI MITATU

SERIKALI ya Rais Jakaya Kikwete imeonywa kwamba kama haitakuwa makini kusimamia vyema mchakato wa kuunda Katiba mpya na kudhibiti mfumuko wa bei katika mwaka huu wa 2012, nchi itayumba.Watu mbalimbali wakimo wasomi na viongozi wa dini, wameuelezea mwaka uliopita wa 2011 kuwa ulijaa matatizo makubwa kisiasa na kiuchumi na kwamba hali hiyo ikiendelea mwaka huu, italeta maisha magumu zaidi kwa wananchi na hata kuiyumbisha nchi.

Mwaka jana Watanzania walishuhudia matukio makubwa ya kisiasa likiwemo lile la kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya huku wabunge wakilumbana kwa hoja motomoto ndani ya Bunge na kwa upande wa pili , vyama vya siasa vikigubikwa na migogoro.Mwaka jana pia Watanzania wameshuhudia mdororo mkubwa wa uchumi huku mfumuko wa bei ukipanda katika miezi ya mwisho na kufikia asilimia 19, hali inayochangia kuongezeka kwa umasikini.Akizungumzia matukio ya kisiasa, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema kuwa mwaka 2011 umekwisha vibaya kutokana na kile alichokiita, mchakato wa katiba kupoteza mwelekeo.
“Ndani ya mwaka 2011, tulitarajia kuwa na mwanzo mzuri wa kupata Katiba mpya hasa baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza azma hiyo na tulianza mchakato vizuri, lakini mwaka umeisha, tumepoteza kila kitu na hii ni hatari,” alisema Bashiru na kuongeza; “Watu walijitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwenye midahalo, lakini Bunge limefanya haraka bila hata kuwashirikisha wananchi”.
Hata hivyo, Bashiru alisema bado hatujachelewa na kumshauri Rais Kikwete kutoendelea na mchakato hata kama amesha saini sheria hiyo ya kuanzisha mchakato wa Katiba. “Bado hatujachelewa, Rais asianze mchakato, asiteue Tume ya Katiba. Ajue kwamba amechaguliwa na wananchi, hata wabunge wamechaguliwa na wananchi, Tume ya Bunge ya Mambo ya Katiba irudi kwa wananchi kuwauliza wanataka nini,” alisema Bashiru.
Akizungumzia matukio ya kisiasa ya Afrika kwa mwaka 2011, Bashiru alisema vita ya kumwondoa aliyekuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddaf imetoa somo kwa nchi za Afrika kwamba hazina uwezo wa kulinda rasilimali zake.
“Tukio la kuondolewa madarakani kwa Kanali Gaddaf limetoa fundisho kwa nchi za Afrika kwamba hazina uwezo wa kulinda rasilimali zake. Nadhani kuna haja ya kuanza kuangalia upya misimamo ya kina Nyerere na Nkrumah,” alisema. Akizungumzia suala la kushuka kwa uchumi hasa kutokana na kuongezeka kwa mfumuko wa bei hadi kufikia asilimia 19 kutoka asilimia tano aliyoikuta Rais Kikwete,alipoingia madarakani mwaka 2005, Bashiru alisema linatokana na kuukumbatia mfumo wa ubepari na siasa uchwara.
“Mfumuko wa bei umeongezeka na bado utaongezeka kwa sababu, tulidanganywa kukumbatia mfumo wa ubepari wa soko huria na siasa uchwara za kubinafsisha kila kitu tukakubali,” alisema Bashiru na kuongeza;“Miaka 26 tangu alipoondoka Mwalimu Julius Nyerere, tumekuwa na siasa uchwara, tunasubiri kila kitu kifanywe na watu wa nje, unategemea nini?” alihoji na kuongeza" Tukoelekea ni kubaya. Akitoa mtazamo wake kwa mwaka mpya wa 2012, Bashiru alipendekeza kuwepo mjadala wa kitaifa wa kubadilisha mfumo wa maisha kutoka katika ubepari uchwara uliopo ili kuwa na mustakabali wa kitaifa, badala ya kuongozwa na matukio.
“Nchi nyingine ipo mijadala rasmi ya mataifa yao. Lakini sisi hapa tunaongozwa na matukio, mara kujivua gamba, mara maandamano Arusha, mara uchaguzi Igunga, hadi mwaka unaisha hakuna tulichofanya zaidi ya kujadili matukio,” alisema Bashiru.
Twalibu
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora wa Afrika (APRM), Rehema Twalibu, alisema japo mwaka uliopita ulikuwa na mwamko mkubwa kutoka kwa wananchi, bado jitihada kubwa zinahitajika katika kuwashirikisha katika mijadala ya kitaifa. “Mwaka huu (2011) umekuwa na mwamko mkubwa kwa wananchi ambapo uelewa wa mambo ya siasa umeongezeka.
Hata hivyo, jitihada zaidi zinahitajika katika kuwashirikisha,” alisema Rehema. Akizungumzia Katiba mpya alisema japo Sheria ya imeshasainiwa na rais, bado wananchi wanahitaji kushirikishwa zaidi kuchangia maoni yao. Kuhusu uchumi, alisema kumekuwa na hali ngumu ya uchumi inayosababishwa na matumizi mabaya ya rasilimali zilizopo.“Bado hatujaweza kutumia rasilimali zetu ipasavyo. Tunazo rasilimali nyingi ambazo kama zitatumika vizuri, hatutakuwa na umasikini huu tulionao,” alisema Rehema.
Askofu Mokiwa
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Dk Valentino Mokiwa aligusia matukio ya kijamii yaliyovuma mwaka 2011 hususan mafuriko yaliyolikumba jiji la Dar es Salaam Desemba mwaka jana. Alisema tukio hilo ni fundisho kwa taifa kutunza mazingira ili kukabiliana na tishio la mabadiliko ya tabia nchi,“Tusiitazame mvua hii kishetani, bali tumtazame Mungu aliyetupa mvua hiyo. Hicho ni kiashiria cha mabadiliko ya tabia nchi. Watu hawayatendei heshima mazingira na bado wanakimbilia kuishi bondeni, hili liwe fundisho kwa mwaka mpya” alisema Dk Mokiwa.
Katika tukio hilo, aliinyooshea kidole serikali akisema kuwa imezembea katika kuwatahadharisha wananchi wanaojenga mabondeni, “Kuna matatizo ya urasimu na uzembe katika idara za mipango miji zinazohusika na ugawaji wa radhi, ndiyo zinasababisha yote hjaya,” alisema.Akitathmini hali ya uchumi nchini, Dk Mokiwa alisema kuwa mwaka uliopita ulitawaliwa na ongezeko la mfumuko wa bei, pengo kubwa kati ya walionacho na wasionacho na gharama za maisha kupanda.
“Hii ni changamoto kwa wachumi wetu, nchi yetu bado ni changa kiuchumi na bado nchi zilizoendelea zinaifanya kuwa jalala la bidhaa zao. Lazima tuwe na mikakati ya kuzalisha bidhaa zetu wenyewe. Tusiogope hata kuwakaribisha wawekezaji wenye uwezo kuja kuwekeza ili kuleta maendeleo,” alishauri.Kuhusu mwenendo wa Bunge kwa mwaka uliopita, alisema kuwa Bunge lilionyesha mifano mibaya kwa jamii kwakuwa na majibizano yasiyokuwa na sababu.
“Bunge lilionyesha picha ya mbaya, kulikuwa na majibizano yasiyo na msingi. Wabunge wajue kwamba bungeni ni mahali patakatifu, siyo mahali pa vurugu. Mikutano ya Bunge ichagie kuimarisha uchumi na maisha ya wananchi, lazima wabunge wawe makini wanapowawakilisha wananchi,” alisema Dk Mokiwa.
Sheikh Mattaka
Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu nchini, Sheikh Khamis Mattaka, alisema kuwa hali ya uchumi imekuwa mbaya kwasababu ya serikali kushindwa kutambua vipaumbele vya kiuchumi, “Uendeshaji wa serikali siyo mzuri, kuna kitu kinaitwa ‘Opportunity cost’, yaani kama unamahitaji mawili kwa wakati mmoja, kwa mfano unataka kununua soda Sh 500 na daftari sh 500, kipi bora? Leo serikali inapoona kuna mahitaji ya ‘ambulance’(gari la kubeba wagonjwa), inakimbilia kununua magari ya kifahari.
Ndiyo maana kila mara taarifa za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonyesha ubadhirifu,” alisema Sheikh Mattaka.Kuhusu suala la Katiba, alitetea sheria ya Katiba iliyosainiwa na Rais Kikwete akisema kuwa wanaoipinga hawaiamini serikali, “Hatuwezi kujenga kama hatuaminiani, hawa wasomi na wanasiasa wanaoipinga sheria hiyo hawaiamini serikali. Mbona sheria nyingi tu zimetungwa hivyo hivyo?” alisema Mattaka.
JK Salamu za mwaka mpya
Katika salamu zake za mwaka mpya kwa taifa jana, Rais Kikwete alisema Tume ya Katiba itakuwa imekamilika ndani ya robo ya kwanza ya mwaka huu na itaanza kazi yake katika robo ya pili au ya tatu ya mwaka huu.

"Ni matarajio yangu kuwa ndani ya robo ya kwanza ya mwaka ujao uundaji wa Tume ya Katiba utakuwa umekamilika. Katika robo ya pili au ya tatu ya mwaka 2012, Tume hiyo itaanza kazi yake ya kukusanya maoni," alisema.

Aliwataka Watanzania wajiandae kushiriki kutoa maoni yao kwa Tume ya Katiba na kuwaonya kujiepusha kuzuia watu kutoa maoni yoa kwa uhuru hasa wale wenye manoni tofuati na serikali.

"Iwe ni mwiko kwa mtu yoyote au kikundi chochote kumzuia mtu au watu wowote kutumia haki yao hiyo. Iwe ni mwiko pia kwa mtu, watu au taasisi yoyote kujaribu kuhodhi mijadala hiyo. Ni vyema tukajua kuwa tunatengeneza Katiba ya watu wote na kwa maslahi yetu sote," alionya Rais Kikwete.

Alisisitiza kwamba serikali yake haina nia ya kutengenezi katiba ya watu fulani wateule au kikundi fulani cha kisiasa au kijamii kwa maslahi yao na kusisitiza watu waachwe watoe maoni yao kwa uhuru.

Kuhusu malimbikizo ya posho za watumishi wa umma, Rais Kikwete alisema anashangaa kuona bado kuna watumishi wanaendelea kuidai serikali wakati alizuia watu kuhamishwa bila ya kulipwa posho zao.

"Bado ningependa kujua imekuwaje tena kuwe na malimbikizo makubwa kiasi hiki. Mambo haya tulikwishaelewana kuhusu namna ya kuepuka malimbikizo. Kulikoni? Je, lini tabia hii ya kulimbikiza madeni itakoma? Nataka majibu toka kwa wahusika," alihoji.

Kuhusu sensa, Rais Kikwete alisema maandalizi ya kufanyika kwa sensa hiyo Agosti mwaka huu yanaendelea vizuri na kwamba maelekezo yatandelewa kutolewa na wajibu wa kila mwananchi.

"Ninawaomba Watanzania wenzangu msikilize maelezo na maelekezo hayo. Pia naomba nyote muhifadhi na kuikumbuka tarehe hiyo ili siku hiyo mtu asikose kuhesabiwa. Mwisho, naomba kila mmoja wetu awepo kuhesabiwa siku hiyo,"alisema

No comments:

Post a Comment