Wednesday, December 21, 2011

Serikali za Mitaa changamoto Zanzibar

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, amesema changamoto kubwa inayoikabili Zanzibar kwa sasa ni kuwapo kwa Serikali za Mitaa.

Akifunga kikao cha ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dar es Salaam jana, Dk. Mwinyihaji alisema hata hivyo suala hilo kwa sasa linafanyiwa kazi na rasimu ya awali ya Sera ya Serikali za Mitaa imeandaliwa.

“Sera hii inaelekeza kufanyiwa kazi kwa maeneo kadhaa ikiwemo kufanya mapitio ya mipaka ya Serikali za Mitaa na hatimaye kuwepo kwa nyenzo sahihi zitakazosaidia kutekeleza majukumu ya serikali hizo,” alisema.

Alisema ofisi yake itaendelea kujifunza njia bora za uendeshaji wa Serikali za Mitaa kutoka OWMTamisemi.

Akizungumzia vikao vya ushirikiano baina ya SMZ na SMT, alisema vikao hivyo vina umuhimu
mkubwa katika kuimarisha Muungano kutokana na kutoa fursa ya kubadilishana uzoefu wa kiutendaji.

“Hiki ni kikao cha nne tangu kuasisiwa kwa vikao hivi, ni dhahiri kila siku vikao vinakuwa na msisimko wa aina yake. Mengi ya yale ambayo yaliwekwa kama malengo yametekelezwa
kwa asilimia kubwa,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment