Wednesday, December 21, 2011

CCM Zanzibar yakerwa na mivutano ya wawakilishi

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema chama hicho kinakerwa na mivutano pamoja na malumbano yaliopo kati ya wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambayo inarudisha nyuma juhudi za wananchi kujiletea maendeleo.

Akizungumza na wandishi wa habari, Vuai alisema malumbano ya aina yoyote kwa watendaji wakuu wa majimbo ya uchaguzi kati ya Mbunge na Mwakilishi kwa sasa hayana nafasi.

“Chama Cha Mapinduzi kinakerwa na mivutano ya aina hiyo katika majimbo ya uchaguzi kati ya Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.....inarudisha nyuma juhudi za wananchi kujiletea maendeleo,” alisema Vuai.

Alisema miongoni wa jambo kubwa ambalo halikutarajiwa kufanyika kwa CCM ni mazungumzo yaliyozaa muafaka na maridhiano ya kisiasa kati ya CCM na CUF na kuzaliwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

“Hili ni jambo kubwa ambalo Chama Cha Mapinduzi kililazimika kukaa meza moja na kukubaliana na CUF kwa lengo la kuzika tofauti za kisiasa na kuwepo maridhiano ya kisiasa......sasa mimi sioni sababu ya kuwepo malumbano kwa Wabunge na Wawakilishi katika majimbo ya uchaguzi,” alisema Vuai.

Alisema ugomvi ni sumu ya maendeleo katika jambo lolote lile na kuwasihi wananchi
kushirikiana na viongozi wao kwa ajili ya kuharakisha maendeleo.

Vuai alizipa kazi kamati ya siasa katika majimbo ya uchaguzi kujadili mivutano hiyo na kuwasilisha ripoti zao ngazi za juu kwa ajili ya maamuzi.

No comments:

Post a Comment