Taarifa za hivi punde za michezo zinasema mshambuliaji wa klabu ya kandanda ya Liverpool, Luis Suarez amesimamishwa kucheza mechi moja na kutozwa faini ya paundi 20,000 na ameonywa kuchunga tabia yake siku zijazo baada ya kukiri mashtaka yaliyoainishwa na Chama cha Soka cha England juu ya utovu wake wa nidhamu.
Suarez hatacheza mechi ya siku ya Ijumaa Liverpool watakapopambana na Newcastle katika uwanja wa Anfield akiwa anatumikia adhabu hiyo. Hivi karibuni Suarez alipewa adhabu ya kufungiwa kucheza kandanda mechi nane kutokana na kosa la kumtusi kwa maneno ya kibaguzi mlinzi wa Manchester United Patrice Evra, amepewa adhabu hiyo mpya ya mechi moja kwa kuonesha ishara ya matusi walipofungwa bao 1-0 na Fulham tarehe 5 mwezi huu.
Aliinua kidole chake cha kati cha mkono wa kushoto wakati akitoka nje ya uwanja.
Klabu ya Liverpool pia imetozwa faini ya paundi 20,000 kwa kushindwa kuwadhibiti wachezaji wake katika mechi hiyo dhidi ya Fulham.
Wachezaji kadha walimzonga mwamuzi Keith Friend wakati kiungo wa timu hiyo Jay Spearing alipooneshwa kadi nyekundu.
Klabu hiyo imekiri makosa yake kwa kushindwa kuwadhibiti wachezaji wake lakini imepinga adhabu ya faini.
Hata hivyo, tume huru ya maadili imesema adhabu ya paundi elfu 20,000 ni sahihi.
Liverpool ilisema hawana cha kusema juu ya adhabu hiyo ya kufungiwa kwa Suarez ama faini iliyopigwa klabu.
No comments:
Post a Comment