Tuesday, December 27, 2011

Zanzibar yapongezwa kuheshimu uhuru wa kuabudu

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imepongezwa kwa kuwa miongoni mwa nchi zenye
kuheshimu uhuru wa kuabudu kwa kiasi kikubwa kwa dini tofauti.

Hayo yalisemwa na Askofu wa Kanisa la Assembles of God (TAG) Tawi la Zanzibar, Dickson Kagonga katika misa ya Krismasi juzi katika Kanisa la Kariakoo mjini Unguja.

Askofu Kagonga alisema uhuru wa kuabudu kwa wafuasi wa dini mbalimbali katika visiwa vya Unguja na Pemba umeipa heshima kubwa Zanzibar ambayo kwa asilimia 97, wananchi wake ni wafuasi wa dini ya Kiislamu.

“Hayo ndiyo sehemu ya mafundisho ya Bwana Yesu ya kuimarisha utulivu na amani ikiwemo kuheshimu maamuzi ya kila mtu,” alisema Askofu Kagonga.

Alisema kama wananchi watapendana na kuheshimiana katika maamuzi ya kila mtu, nchi itapata baraka na neema kubwa kutoka kwa Mola muumba na kuondokewa na majanga
mbalimbali mabaya yanayotisha.

Aliwataka wananchi wa Unguja na Pemba kudumisha amani na utulivu uliopo sasa ambao unatoa nafasi ya kila aina kwa wananchi kufanya shughuli zake bila ya bughudha ikiwemo
kuabudu chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Mapema kuhusu maoni yake marekebisho ya Katiba, alisema Mfumo wa Serikali mbili uliopo sasa ni mzuri ambao kwa kiasi kikubwa unatoa nafasi ya kuwepo kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alisema mfumo wa Serikali moja kwa Zanzibar haufai hata kidogo kwa sababu utaimeza Zanzibar na hivyo moja kwa moja kuathirika kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Mimi kwa maoni yangu bado napenda kuwepo kwa muundo wa Serikali mbili ambao ni mzuri kwa sababu unaimarisha Muungano na sio Serikali moja ambao utalimeza taifa la Zanzibar,” alisema Askofu Kagonga.

No comments:

Post a Comment