Wednesday, January 11, 2012

BAADA YA KUCHEZEA KICHAPO KUTOKA KWA AZAM SIMBA WA JITETEA


Kocha Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic ‘Profesa Chico’.

KOCHA wa Simba, Milovan Cirkovic amesema safu ya ulinzi ya timu yake ndiyo imewafanya wachapwe na Azam mabao 2-0.
Simba ilikubali kichapo hicho kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi uliopigwa katika Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar juzi.
Vijana hao wa Msimbazi ambao walikuwa mabingwa watetezi wa kombe hilo, wameshindwa kukamilisha ndoto zao za kulitwaa  taji hilo kwa mara ya pili mfululizo.
Akizungumza  kwa masikitiko jana asubuhi, Milovan alisema licha ya kikosi chake kucheza vizuri kwa mara ya kwanza tangu alipoanza kukinoa, amechukizwa na makosa ya kizembe waliyofanya walinzi wake.
 “Kwa mara ya kwanza naweza kusema kidogo timu ilicheza vizuri, lakini tatizo bado lipo katika ukuta, wameendelea kuonyesha makosa yaleyale waliyokuwa wanayafanya katika michezo iliyopita licha ya kuwapa maelekezo ya kutosha mazoezini.
“Nilitegemea kupitia mazoezi hayo, Kelvin (Yondani) na Victor (Costa), wangeonyesha kiwango kizuri, lakini hali imekuwa tofauti, sasa utagundua kuwa bado kuna kazi inatakiwa kufanyika, lakini sikati tamaa, nitaendelea kuwaelekeza na leo (jana) nimepanga kuongea nao ili kujua nini tatizo lao,” alisema Milovan raia wa Serbia.
Simba ambayo mwaka jana ilifanya vizuri kwenye michuano hiyo inajiandaa na michuano ya Kombe la Shirikisho ambayo inatarajia kucheza na Kiyovu ya Rwanda kati ya Februari 17 hadi 19 jijini Kigali.

No comments:

Post a Comment