Samwel Sitta
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Ismail Jussa Ladhu, amemshambulia Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kwa kuwaingiza katika orodha ya maadui wasioitakia mema Zanzibar.
Jussa, alimshambulia Waziri Sitta kupitia hotuba yake iliyorekodiwa katika mkanda wa video uliosambazwa jimboni kwake.
Jussa alisema iwapo katiba mpya haitatoa Muungano wa haki wa Tanganyika na Zanzibar, basi itakuwa ni katiba ya Tanganyika na si ya Muungano.
Alisema akiwa Kaimu Waziri Mkuu katika Mkutano wa Nne wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sitta alizungumzia mambo matatu yaliyoonekana kuidharau Zanzibar na kuzidi kuikandamiza.
Alisema mambo hayo yalikuwa ni kuhusu umeme, mafuta na muundo wa Muungano.
Jussa alisema Waziri Sitta alisema, Zanzibar ina deni la karibu Sh. bilioni 50 la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), lakini hakuna mtu, ambaye amekuwa akipiga kelele kwa sababu mambo hayo yanazungumzika katika Muungano.
Alisema Zanzibar ilipaswa kulipwa kutokana na kuwekeza nguvu zake za fedha katika mradi wa umeme wa Kilomo uliopitia Bagamoyo.
Jussa alisema kusema Wazanzibari wanabebwa ni madai ya uongo, kwani Zanzibar hawajazoea kubebwa na kwamba, kama wanawabeba basi wawatue.
Alisema hata Mwalimu Nyerere alijua Zanzibar ilikuwa ni nchi iliyokuwa ikijitegemea kwa wataalamu wake wazalendo baada ya Uhuru.
Jussa alisema Zanzibar ilipopata uhuru wake haukuwa wa ‘kubebwabebwa’, bali ilikuwa ikiongoza katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kuwa na wataalamu wazalendo.
“Kuonyesha kwamba hawa wenzetu hawana nia njema nasi, mwaka 2010 Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji) ilitangaza ongezeko la bei ya nishati ya umeme. Kwa Bara wakaongeza asilimia 21, lakini huku Zanzibar ikawa zaidi ya asilimia 100. Sasa wanatupenda hawa au wanataka kutuua?” alihoji.
Alisema Ibara ya 132 na 133 zinataja Tume ya Pamoja ya Fedha na Akaunti ya Muungano, lakini upande wa Tanzania Bara bado ulikuwa hautaki kutekeleza.
Jussa alisema Sitta alipotosha kwa kusema Muungano wa serikali tatu ungevunja muundo wa sasa wa Muungano.
Alisema Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikha Abeid Aman Karume, alitaka serikali moja, lakini Mwalimu Nyerere akatumia busara kuibakisha Zanzibar.
“Nampa changamoto Sitta. Atueleze ni lini na wapi mzee Karume alitaka muundo wa Muungano wa serikali moja? Yeye anarejea maneno ya Nyerere. Huyo Nyerere mwenyewe hakuwahi kusema maneno hayo wakati mzee Karume akiwa mzima, mbona alisema alipouawa..., yeye alikuwa adui wa Zanzibar.”
Alisema kwa jinsi anavyomfahamu, Karume alikuwa ni mzalendo asiyeweza kuisaliti Zanzibar na kuifanya imezwe.
Jussa alisema hotuba za Karume hadi leo zipo na kwamba, aliwahi kusema Muungano ni kama shati “ukitubana tutalivua.”
Alisema Mwalimu Nyerere aliunda Muungano kwa siri kubwa akishirikiana na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu (AG) wakati Tanganyika ikipata uhuru kutoka kwa Uingereza aliyefahamika kwa jina la Rowland Brown.
Jussa alisema Brown aliandaa muundo wa Muungano kama wa Uingereza na Ireland ya Kaskazini, ambayo ilikuwa koloni lake.
“Sasa sisi ni mateka wa Tanganyika? Kama hakutakuwa Muungano wa haki na kuheshimiana Wallah tutaukata. Eti Sitta anasema Nyerere alitupenda sana, angetuletea mfumo huu wa kikoloni?”
Alisema Waziri Sitta alikosea kusema mafuta yako katikati ya bahari na kwamba, hata kama ikitokea bahati Muungano ukivunjika, bado jambo hilo litapaswa kuzungumzwa, hayakuwa ya kweli.
Jussa alisema mafuta yaliyopo katika eneo la bahari karibu na Zanzibar yako kwenye visiwa hivyo.
Jussa alisema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limegawa vitalu vya kufanya utafiti wa mafuta kuanzia Mtwara hadi Zanzibar.
Alisema kitalu namba 8 kiko katika eneo la bahari la kisiwa hicho, wakati kitalu namba 9, 10 na 11 vimegawiwa kwa Kampuni ya Shelli ya Uingereza inayofahamika kwa kazi ya utafiti wa mafuta duniani.
NIPASHE iliwasiliana na Sitta, ambaye alisema: “Naendelea kuutafuta. Maana nimeusikia tu. Lakini kama ni kweli maneno hayo yametolewa na mwakilishi ni hatari.”
Aliongeza: “Mwakilishi anaweza kumtukana Baba wa Taifa na mimi, ambaye nilikuwa spika na sasa waziri katika serikali ya Muungano? Haya mambo yanazungumzwa kwa busara.”
No comments:
Post a Comment