Saturday, February 18, 2012

Jussa aipalia makaa CUF

SIKU chache baada ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu, kudai kuwa chama hicho kilifanya vibaya katika uchaguzi mdogo wa jimbo la uwakilishi la Uzini kwa sababu jimbo hilo lina Wakristo wengi na watu wa bara wengi, wadau mbalimbali wamemponda wakidai ni mbaguzi.
Jussa ambaye pia ni mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe visiwani Zanzibar, alitoa madai hayo juzi, wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha Mlimani.
Katika uchaguzi huo ambao mgombea wa CCM, Mohammed Raza, aliibuka mshindi kwa kupata kura 5377, CUF ilidondoshwa na CHADEMA katika nafasi ya pili iliyojikusanyia kura 281 dhidi ya kura 223 za chama hicho.
Kauli ya Jussa ililalamikiwa na wananchi wengi waliotoa mawazo yao kupitia mitandao ya kijamii, wakisema moja kwa moja anataka kuashiria kuwa chama chake kinaungwa mkono visiwani pekee na na penye Waislamu.
Wachangiaji hao wakiwemo wanachama wa CCM, walidai kuwa Jussa analenga kuonyesha ni jinsi gani chama hicho kilivyo cha kibaguzi kama alivyokituhumu aliyekuwa mwanachama wao, Hamad Rashid Mohamed, mbunge wa Wawi.
“Nimehudhuria mikutano ya ufunguzi ya vyama vyote vitatu vikubwa vilivyoshindana katika uchaguzi ule, kwa maana ya CHADEMA, CCM na CUF na kila jioni nilikuwa najua kila kilichozungumzwa kwenye mikutano ya vyama hivyo viwili, hata kama sikuhudhuria ila nilishangaa kumsikia Jussa kuwa walishindwa kwa sababu kule kuna Wakristo wengi na watu wengi wa kutoka bara,” alisema mchangiaji mmoja.
Alisema kauli ile imezidi kumwanika Jussa kuwa ni mwanasiasa wa namna gani na kwamba vibaya kumsikia kiongozi kama yeye, akizungumza maneno hayo.
“ Jussa anataka kuwaambia Watanzania kuwa CUF wanaweza kushindana na kushinda pale tu ambapo kuna Waislamu wengi na misikiti mingi, kwamba penye Wakristo wengi, makanisa mengi, CUF haiwezi kushindana kwa dhati na kushinda au popote ambapo kuna watu wengi wa bara, CUF haiwezi kushindana na kushinda uchaguzi,” alihoji mchangiaji huyo kwenye mtandao wa kijamii.
Alisema kuwa Jussa anataka kuwasukuma Watanzania waamini katika propaganda za CCM zinazopalilia ubaguzi ndani ya jamii, kuwa CUF ni chama cha Waislamu na kuwa CUF ni chama cha Zanzibar.
Mchangiaji mwingine toka Zanzibar alisema kuwa kauli ya Jussa inajidhihirisha wazi kuwa ni mdini kwani hata wakati wa kampeni kule Uzini CUF walikuwa wakitembea na makaratasi waliyoita ni waraka wa maaskofu, wakiwadanganya wananchi kuwa unasema CHADEMA ni chama cha Wakristo.
“Nakumbuka ambavyo Jussa alitumia takriban asilimia 80 ya muda wa hotuba yake siku ya uzinduzi wa kampeni ambayo alikuwa mzungumzaji mkuu, kuizungumzia CHADEMA. Akaonyesha kushtushwa sana na nguvu ambayo chama hicho kiliyoionyesha katika uchaguzi huo.
Akahoji kulikoni. Kisha akaingiza propaganda, akisema kuwa nguvu hiyo ilikuwa na ajenda ya siri ya kusababisha vurugu Zanzibar, eti kama ambavyo kimekuwa kikifanya bara,” alisema mchangiaji huyo.
Hata hivyo, wakati Jussa akitoa kauli hiyo, mbali na Raza pia mbunge wa Jamhuri ya Muungano kutoka jimbo hilo, Sief Khatib (CCM), ni Muislamu aliyechaguliwa na hao anaowaitwa Wakristo.
Kada mmoja wa CCM ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, aliliambia gazeti hili jana kuwa anajipanga kumwanika Jussa na chama chake kutokana na uzushi wa kutaka kupandikiza chuki za udini nchini.

No comments:

Post a Comment