Saturday, February 18, 2012

Nape: Mleteni Slaa Arumeru • ASEMA CCM WANAKESHA WAKIOMBA ARUHUSIWE

SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, kusema ni ruksa kwa Katibu Mkuu wao, Dk. Willibrod Slaa, kugombea ubunge katika jimbo la Arumeru Mashariki, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimejibodoa kuwa kinamsubiri kwa hamu.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, alisema kuwa CCM wanaomba usiku na mchana Dk. Slaa agombee katika jimbo hilo ili wamalize kazi ya uchaguzi mkuu 2015.
Kwa kujiamini, Nape alisema kuwa Dk. Slaa akitia mguu Arumeru Mashariki, haponi, hivyo utakuwa mwisho wake kisiasa na umaarufu wa CHADEMA.
“Dk. Slaa ndiye jembe la CHADEMA, akija Arumeru Mashariki, tutahakikisaha tunalikata makali na tukishafanya hivyo hawezi tena kuwa maarufu mwaka 2015 na chama kizima hakitakuwa na nguvu, hapo kazi yetu ni nyepesi kama kumsukuma mlevi,” alisema Nape.
Alipoulizwa endapo kauli hiyo ni ya woga dhidi ya Dk. Slaa ili kiongozi huyo asiende Arumeru, Nape alijibu kwa kujiamini kuwa CHADEMA ikitaka kuthibitisha hilo, imlete kigogo huyo katika jimbo hilo.
Aliongeza kuwa umaarufu wa CHADEMA unatokana na mtu mmojammoja kama Dk. Slaa na kutamba kuwa kiongozi huyo ni maarufu awapo bungeni, hivyo watahakikisha anashindwa ili uwe mwisho wake kisiasa na chama chake.
Hata hivyo, pamoja na kauli hizo za majigambo ya Nape, Dk. Slaa amekwishatoa msimamo wake kwamba hakakuwa tayari kuwani ubunge katika jimbo lolote kwa wakati huu.
Tangu kuanza kwa harakati za kuwania ubunge katika jimbo hilo, Dk. Slaa amegusa hisia za wasomi wanaharakati na makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo wafuasi wa chama chake, wakimtaka agombee kiti hicho.
Matakwa hayo ya kumtaka Dk. Slaa agombee, yanatokana na imani kwamba kulingana na umaarufu aliojijengea na rekodi yake ya utendaji wenye audilifu, CHADEMA haitapata ushindani mkubwa toka kwa CCM.
Itakumbukwa kuwa Dk. Slaa aligombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita na kukonga nyoyo za Watanzania wengi ambao hadi sasa wanaamini kuwa aliibuka mshindi ila kura zake zilichakachuliwa.
Hisia za wanaotaka Dk. Slaa agombee ubunge katika jimbo hilo, zimechochewa zaidi na kauli ya Mbowe, aliyekaririwa na gazeti moja akisema kama kiongozi ataamua kuwania kiti hicho, CHADEMA itaheshimu uamuzi wake.
Mbowe pia alisema kama Dk. Slaa hatakuwa tayari, chama vilevile hakiwezi kumlazimisha kugombea. Akitamba kuwa hana shaka ya kukubalika kwake na imani aliyojijengea mwanasiasa huyo kwa Watanzania.
Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa katika kuteua mgombea, CHADEMA inazingatia vigezo na si suala la uteule.
Na wakati akisema hivyo, aliyekuwa mgombea ubunge katika jimbo hilo katika uchagzu mkuu uliyopita, Joshua Nasari, alisema endapo Dk. Slaa ataamua kugombea na chama kikampitisha, ataridhia.
Uchaguzi huo unaotarajia kufanyika Aprili mosi mwaka huu, umetokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jermiah Sumari (CCM).
Tayari harakati za kuchukua fomu zimeanza ndani ya vyama vya siasa huku kila kimoja kikitamba kulinyakua hasa mchuano mkali uko kwa CCM na CHADEMA vinavyopewa nafasi kubwa ya ushindi.

No comments:

Post a Comment