Tuesday, February 14, 2012

Posho mpya za wabunge zafutwa

HATIMAYE nyongeza ya posho za vikao vya wabunge kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 zimefutwa, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema.

Kauli hiyo rasmi kutoka kwa kiongozi wa Bunge imekuja baada ya kuwepo kwa taarifa za kutatanisha kuhusu posho hizo baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Spika wa Bunge Anne Makinda kutangaza kwamba, tayari Rais Jakaya Kikwete aliziidhinisha  lakini, Ikulu ikakanusha.
 
Januari 31, Ikulu ilitoa taarifa hiyo ikisema, "Maelezo ya Rais Kikwete kuhusu suala hilo yako wazi na hakuna mahali ambako amebariki posho hizo," lakini siku hiyo mchana Spika Makinda, "Siyo tutaanza kulipa, tayari tumekwishaanza kulipa."

Jana, akizungumza na Mwananchi kwa njia ys simu, Ndugai alisema posho hizo hazijawahi kulipwa kwa kuwa Rais hajatoa kibali cha kufanyika hivyo.

Ndugai alisema kibali kilichopo ni cha malipo ya posho za zamani ambazo hata yeye mpaka sasa analipwa huku akisisitiza, hajawahi kulipwa hata senti moja ya posho hizo mpya zilizoibua mjadala mpana nchini.

"Hakuna cha Spika alisema hapo, Ikulu imeshasema Rais hajasaini hivyo zitaendelea kulipwa zile za zamani kwa kuwa ndizo zenye kibali," alifafanua  Ndugai na kuongeza; "Hata mimi sijalipwa hizo posho mpya hivyo, hakuna kitu kama hicho."

Alisema ili posho hizo ziweze kulipwa ni lazima Rais atie saini kibali cha kuziruhusu, ndiyo itawezekana kufanyika hivyo.

Sakata na kauli tata

Taarifa za wabunge kuongezewa posho hizo za vikao ziliripotiwa kwa mara ya kwanza na gazeti hili mnamo mwezi Novemba, ambazo ni kutoka Sh70,000 hadi 200,000 kutwa hivyo kufanya bajeti ya posho hizo kwa mwaka kufikia Sh28 bilioni.

Kutokana na ongezeko hilo, kila mbunge atakuwa akilipwa Sh 80,000 kama posho ya kujikimu (per diem) anapokuwa nje ya jimbo lake, posho ya vikao Sh200,000 na mafuta ya gari Sh50,000 kila siku, sawa na Sh330,000 kwa siku huku mshahara jumla kabla ya makato ukielezwa kuwa ni sh 2.3 milioni.

Kwa mujibu wa Dk Kashillilah, mapendekezo ya kutaka posho za wabunge zipande, yaliibuka katika mkutano wa wabunge mjini Dodoma Novemba 8 mwaka jana, lakini hadi wakati anatoa tamko alisema yalikuwa hayajaanza kutekelezwa.

Siku kadhaa baadaye, Spika Makinda akaibuka na kauli inayoonekana kupingana na ile ya Katibu wake na akakiri kuwa ni kweli posho za wabunge zilikuwa zimeongezeka kutoka Sh70,000 hadi Sh 200,000 kwa kikao na zilikuwa zimeanza kutumika.

"Mbunge huyo alikuwa anapata Sh 70,000 kwa hiyo tumemwongezea Sh130,000 na hupati 'unless' (isipokuwa) umefanya kazi ya Bunge na umesaini asubuhi na jioni hujafanya hivyo hupati hizo hela, alisema Makinda katika kauli inayokinzana na ile ya Dk Kashillilah ambaye wanafanya kazi katika ofisi moja.

Hata hivyo, Ikulu nayo ikaja kuibuka ikisema, "Kwanza, Rais Kikwete anakubali haja ya kuangalia upya posho kwa wabunge lakini amewataka wabunge kutumia hekima na busara katika kulitafakari suala hili. Pili, Rais Kikwete amewataka Wabunge kutumia Kikao cha sasa cha Bunge kulizungumza upya suala hilo."

Utata huo wa kauli toka kwa watendaji wakuu wa taasisi hii nyeti ya Bunge ndio ulioongeza kasi ya mjadala wa nyongeza za posho za wabunge. Waliopata fursa ya kuchangia wanahoji sababu ya kukinzana kwa majibu katika suala nyeti kama hilo.

Wengine wanaenda mbali zaidi kwa kusema utata huo unaonyesha ni jinsi gani suala hilo lilivyo tata na ambalo huenda likawa halikuwa na ‘baraka’ hata na baadhi ya watendaji hao na kwamba utekelezaji wake huenda umepelekwa haraka haraka bila kupata baraka za wahusika.

mwisho

No comments:

Post a Comment