SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa sh milioni 50 kusaidia katika kuendeleza makazi mapya ya watu waliolazimika kuhama kutoka mabondeni baada ya maafa ya mafuriko katika jiji la Dar es Salaam Desemba mwaka jana.
Hundi ya fedha hizo, ilikabidhiwa kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Iddi, jana mjini Dodoma.
Akikabidhi fedha hizo, Balozi Iddi alisema msaada huo ni muendelezo wa kusaidiana baina ya pande mbili za Muungano.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeguswa na kusikitishwa na tukio la kutisha la maafa ya mafuriko lililotokea ghafla na kuwakumba wananchi wa Dar es Salaam,” alisema.
Aliongeza kuwa walipokea kwa huzuni taarifa za kupoteza watu wengi na mali zao na hasara ya nyumba nyingi zilizoathiriwa na mafuriko hayo ambayo yaliwaacha watu wengi bila makazi.
“Hivyo, kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, napenda kuwasilisha mchango wetu wa sh milioni 50, kusaidia mchakato wa kuwasitiri waathirika wa mafuriko hayo,” alisema.
Waziri Mkuu Pinda alishukuru kwa msaada huo na akawashukuru wananchi waliokuwa wakiishi mabondeni, hasa eneo la Jangwani kwa kuukubali mpango wa serikali wa kuwahamishia kwenye maeneo yasiyo hatarishi.
Watu wapatao 40 walifariki na mamia wengine kukosa makazi baada ya kubomolewa na nyumba zao kutokana na mafuriko hayo.
No comments:
Post a Comment