SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza kuyafanyia ukarabati majengo ya magereza yaliyopo Unguja na Pemba na kuongeza huduma zinazokwenda na wakati na kulinda haki za binadamu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame alisema hayo juzi wakati alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu malengo na mikakati ya wizara yake katika kipindi cha miezi sita ijayo.
Alisema hali ya magereza imekuwa nzuri na huduma mbalimbali muhimu zenye lengo la kuimarisha haki za binadamu zinapatikana.
Dk. Mwinyihaji alisema katika taarifa iliyowasilishwa ya haki za binadamu na utawala bora, mambo mengi yaliyotajwa katika ripoti hiyo yameanza kutekelezwa kwa vitendo.
Kwa mfano alisema wafungwa watoto wanaotumikia adhabu mbalimbali magerezani kwa sasa wametenganishwa na watu wazima kwa lengo la kulinda haki za watoto na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.
“Tumeanza kuimarisha huduma nzuri katika Magereza yetu ya Unguja na Pemba kwa lengo la kuimarisha haki za binaadamu na utawala bora,” alisema.
Kuhusu chakula cha wafungwa, alisema wanapata chakula bora kutwa mara tatu pamoja na mahitaji mengine muhimu ikiwemo matibabu.
Dk. Mwinyihaji alisema ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliitaka SMZ kuimarisha Magereza kwa lengo la kuimarisha Utawala Bora na Haki za Binadamu.
No comments:
Post a Comment