WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Said Ali Mbarouk amewataka wavuvi na wananchi wa maeneo ya pwani kuacha kuvua samaki aina ya kasa ambao kwa sasa wapo katika hatari ya kutoweka duniani.
Mbarouk alisema hayo wakati alipovitembelea vikundi vya wavuvi na wananchi wanaojishughulisha na kuendeleza mazao ya baharini ikiwemo chaza, mwani pamoja na kasa.
Alisema hivi karibuni yamejitokeza matukio mbalimbali yanayoonesha kuwepo kwa vifo vinavyotokana na wananchi kula nyama ya kasa wakati Idara ya Maendeleo ya Uvuvi imepiga marufuku.
“Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepiga marufuku uvuvi wa samaki aina ya kasa kwa sababu mbalimbali... moja kubwa ni kwamba viumbe hao wapo katika hatari ya kutoweka duniani,” alisema Mbarouk.
Alisema jumuiya za kimataifa zimepiga marufuku uvuvi wa kasa ambapo kwa Zanzibar marufuku ya uvuvi huo ipo kwa wananchi na wavuvi wote.
Alisema katika uvuvi wa kasa, tayari matukio manne yametokea mwaka jana hadi mapema mwaka huu ambapo watu 16 wamefariki baada ya kula nyama yake anayesadikiwa kuwa na sumu huko Tumbe Pemba.
Alisema matukio ya vifo vya watu kula nyama ya kasa vimezua hofu kubwa huku wananchi wengine wakihusisha kasa hao kudungwa sindano.
Zipo aina ya kKasa wapatao 10 ambapo wapo baadhi yao hawafai kwa matumizi ya kula huku wakiwa na sumu kali inayosababisha vifo.
Mapema, Mbarouk aliwataka wananchi na wavuvi pamoja na wanavikundi mbalimbali kujikusanya na kuibua miradi itakayoongeza kipato katika maeneo yao. Alisema kwa mfano wananchi wanayo fursa kubwa ya kufuga samaki wa aina mbalimbali ikiwemo kamba ambao kwa sasa soko lake la ndani pamoja na nje ni kubwa.
No comments:
Post a Comment