Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima linalomilikiwa na kampuni ya Free Media, Absalom Kibanda, akisindikizwa na Polisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana.
Kibanda, jana aliunganishwa kwenye kesi ya kushawishi askari polisi, magereza na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutoendelea kuitii serikali yao ambayo inamkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Arusha, Samson Mwigamba.
Ameunganishwa kwenye kesi hiyo kufuatia kuruhusu kuchapishwa makala iliyokuwa na kichwa cha habari cha “Waraka maalum kwa askari wote” iliyochapishwa katika gazeti la Tanzania Daima toleo la Novemba 30, mwaka huu.
Alisomewa shtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Stewart Sanga, ambapo upande wa mashtaka uliongozwa na Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda.
Kaganda alidai kuwa, Mwigamba na Kibanda kwa pamoja Novemba 30, mwaka huu, walichapisha makala hiyo kwa nia ya kuchochea mamlaka halali ya serikali zilizopo kwa mujibu wa sheria ambazo ni askari polisi, magereza na askari wa JWTZ.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, Kibanda alikana kutenda kosa hilo na aliachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya dhamana hadi Januari 19, mwakani.
Kabla ya kumpa dhamana, mahakama hiyo ilimtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili, hati ya nyumba, kusaini bondi ya Shilingi milioni tano, kuwasilisha hati ya kusafiria na kuripoti polisi kila mwisho wa mwezi.
Hakimu Sanga alimtaka Kibanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kuhudhuria mahakamani hapo Januari 19, mwakani akiwa na mshtakiwa mwezake Mwigamba.
Mwigamba alishindwa kufika mahakamani hapo jana kwa kuwa ana kesi nyingine mkoani Arusha.
Katika kesi hiyo, Kibanda anatetewa na jopo la mawakili wanne akiwemo Deogratius Ringia, Isaya Matambo, Juvenalis Ngowi na Nyaronyo Mwita Kicheere.
Upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Waandishi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini walifurika mahakamani hapo kusikiliza kesi hiyo.
Desemba 8, mwaka huu, Mwigamba alipandishwa katika mahakama hiyo kujibu shtaka la kuandika makala hiyo.
Kaganda alidai mbele ya Hakimu Lema kuwa, mshtakiwa aliandika waraka huo akiwa na nia ovu ya kushawishi na kuchochea Jeshi la Polisi, Magereza na Jeshi la Ulinzi kuvunja sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutokutii serikali iliyoko madarakani.
Kibanda kabla ya kufikishwa mahakamani jana, alihojiwa katika makao makuu ya Jeshi la Polisi kwa siku mbili Ijumaa iliyopita na jana kuhusiana na makala hiyo.
No comments:
Post a Comment