Mbunge wa Jimbo la Wawi (CUF), Hamad Rashid, akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, kuhusu wito wa kutakiwa kuhudhuria kikao cha Kamati ya Nidhamu na Maadili ya chama chake. (Picha na Omar Fungo)
Siri hizo ambazo ziliwekwa hadharani jana na Hamad, baadhi zilifichuliwa kutoka kwenye waraka wa ndani (internal memo) wa CUF na nyingine kutoka kwenye ujumbe wa barua pepe uliotumwa kupitia mtandao wa kompyuta (internet).
Kwa mujibu wa Hamad, njama za kutaka kufukuzwa kwake katika CUF, zilibainika kupitia ujumbe huo wa barua pepe ulioandikwa na Maalim Seif kwenda kwa Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye yuko nje ya nchi Desemba 14, mwaka huu.
Sehemu ya barua pepe hiyo inaeleza: “Yeye (Hamad) muono wetu tumfukuze kwenye chama na akiamua kwenda mahakamani na mahakama kutoa maamuzi ya kumpendelea yeye mwache awe mbunge wa mahakama kama walivyokuwa akina Asha Ngede na Naila Majid.
“Wanachama walio wengi wanatudadisi kwanini hatuchukui hatua. Sisi ni kumuachia jamaa yako aendelee kufanya kazi aliyopewa na rafiki yake ya kukivuruga chama, au chama kimvuruge yeye. Ikishajulikana kuwa si mwanachama tena, atakuwa hana mashiko. Muache aende CCM au Chadema akawe mgombea mwenza.”
Hamad anasema pia kuhusishwa kwa harakati zake na Lowassa, kulifanywa kupitia waraka wa ndani ya chama, wenye kichwa cha habari: “Kuchafuka kwa hali ya kisiasa ndani ya chama.”
Anasema waraka wa ndani ya chama uliandikwa na Mkurugenzi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya CUF Taifa, Hamis Hassan, kwenda kwa Profesa Lipumba, Desemba 4, mwaka huu.
Hamad alifichua siri hizo alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, muda mfupi baada ya kukutana na Kamati ya Nidhamu na Maadili ya CUF, katika ofisi za chama hicho.
Katika mkutano huo, Hamad pia aligawa kwa waandishi wa habari nakala zenye ujumbe huo wa barua pepe na zile za waraka huo wa ndani wa CUF.
HAMAD AGOMA KUHOJIWA
Katika kikao na Kamati ya Nidhamu na Maadili jana, Hamad alikataa kuhojiwa na kamati hiyo kwa madai kwamba haiko kikatiba ya chama na pia hana imani na wajumbe wake watano kati ya wanane, akiwamo Mwenyekiti wa kamati kwa vile walikwishamtolea hadharani tuhuma dhidi yake na kumtia hatiani kabla ya kupewa fursa ya kusikilizwa.
Hamad alieleza kuwa, kwenye kikao na kamati hiyo jana, aliomba apewe tuhuma zake kwa vile barua ya wito aliyoandikiwa inaeleza kuwa aende kujieleza tuhuma za kwenda kinyume cha katiba ya chama, hivyo akataka aelezwe ni vifungu vipi vya katiba alivyokwenda kinyume navyo.
Hata hivyo, alisema aliambiwa kuwa jambo hilo atasomewa baadaye.
Alisema pia aliomba apewe kumbukumbu za hadidu rejea ya kikao kilichounda kamati hiyo, lakini akaelezwa pia kuwa hilo nalo litapatikana baadaye.
Hamad alisema, pia aliomba apewe kanuni zitakazotumika kuendesha shughuli yote ya kujibu tuhuma hizo, lakini nazo pia akaahidiwa kuwa atapewa baadaye.
“Lakini mimi nilitanguliza jambo moja la ziada. Nikasema hii kamati mimi siikubali, kwanza haipo kikatiba, lakini pia wajumbe wake siwakubali,” alisema Hamad.
Alitoa sababu za kutokuwakubali wajumbe hao, akisema kwanza Mwenyekiti wa Kamati, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CUF Taifa, Machano Khamis Ali, hamtaki kwa sababu alishiriki kikamilifu katika kutengeneza tuhuma dhidi yake na kumtia hatiani katika vikao mbalimbali.
Alisema miongoni mwa vikao vilivyotumiwa na Machano kumtuhumu na kumtia hatiani, mbali ya kimojawapo cha Baraza Kuu la Uongozi wa CUF Taifa alichotamka kwamba, walimfukuza James Mapalala na wengine na wataendelea kuwafukuza wengine, ni kile kilichofanyika kati ya viongozi na wanachama katika ofisi za CUF Buguruni, hivi karibuni.
Hamad alisema katika kikao hicho cha Buguruni, Machano alitamka:“...Nitawashughulikia (kina Hamad na wenzake).”
“Sasa ukishafika hapo na wewe ndio mwenyekiti tena, kwa kweli sioni kama utafanya haki. Lakini nataka nimshukuru sana, baada ya kulisema hilo aliliona uzito wake. Alisema mimi kama jaji mwadilifu nisingeweza kuendelea na kikao,” alisema Hamad.
Alisema mjumbe mwingine aliyemkataa ni Hamis Hassan, ambaye ni Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Mjumbe wa Kamati Tendaji ya CUF Taifa. Hamad alisema alimkataa Hamis kwa vile ndiye muandaaji wa tuhuma zote dhidi yake.
Alisema Hamis alimwandikia Profesa Lipumba waraka wa ndani ya chama, Desemba 4, mwaka huu, akielezea juu ya kuchafuka kwa hali ya kisiasa ndani ya nchi na namna baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi walivyokwenda kwenye kikao cha baraza wakiwa na ajenda ya kutaka kumng'oa mwenyekiti, katibu mkuu na makamu mwenyekiti.
Alisema pia Hamis katika waraka huo, ameorodhesha wanachama wengi na kuwashutumu kuwa ni waasi ndani ya chama na kumweleza Profesa Lipumba kuwa wahuni 150 kwenye tawi la Chechnya, Mabibo, kwamba, Hamad aliwalipa fedha ili wawapige Blue Guard bila kushauriana naye (Hamad), huku akijua wazi kuwa hakukuwa na ugomvi wowote tawini hapo.
AHUSISHWA NA LOWASSA
Alisema pia Hamisi anadai katika waraka huo wa ndani ya chama kuwa Hamad anashikiriana na Lowassa kumvuta kasi ili agombea urais kupitia na yeye (Hamad) awe Mgombea Mwenza wake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa madai kwamba uwezekano wa Lowassa kupata nafasi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni mdogo.
Hata hivyo, Hamad alisema hana ukaribu na Lowassa kulinganisha na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na kwamba, ukaribu wake na Lowassa ni kuwasalimiana tu.
KAULI YA LOWASSA
NIPASHE iliwasiliana na Lowassa jana na baada ya kuelezwa madai hayo kwa kirefu, alijibu: “Niache kidogo, niko msibani kijijini.”
“Lakini baya zaidi (Hamis) akamwambia mwenyekiti kwamba sisi tuko tayari hata kuua ili tupate nafasi ya uongozi. Hizi ni tuhuma nzito sana,” alisema Hamad.
Alisema alichokifanya kwenye kamati jana, aliusoma waraka huo wa ndani ya chama mbele ya kamati kumkataa Hamis.
Hamad alisema pia aliwakataa wajumbe wa Kamati Tendaji ya Chama waliochaguliwa kuingia ndani ya Kamati ya Nidhamu na Maadili.
Alisema Kamati Tendaji kupitia kwa Mwenyekiti wake, Maalim Seif ndiyo iliyochagua wajumbe wa Kamati ya Nidhamu na Maadili wakati Kamati Tendaji tayari ilikwisha kuwa na maamuzi dhidi yao (kina Hamad).
Hamad alisema ushahidi wa hilo unathibithswa na barua pepe ya Desemba 14, mwaka huu, iliyoandikwa na Maalim Seif kwenda kwa Profesa Lipumba, yenye kichwa cha habari: “Tuwe waangalifu tusiingie kwenye mtego”, ikieleza kwamba alishauriana na Machano na kuona kuna haja ya Hamad na kundi lake kuitwa katika Kamati ya Nidhamu na Maadili kuhojiwa na kufukuzwa kwenye chama.
MAALIM SEIF
Alipoulizwa, Katibu wa Maalim Seif, Mohamed Nuru, alisema bosi wake amesema hafikirii kama ni jambo sahihi kujibizana kwenye vyombo vya habari kwa vile chama kina vikao.
HAMIS
Kwa upande wake, Hamis, alisema walimuita Hamad na yeye akaitikia wito, hivyo kuzungumza mambo ya kamati kwenye vyombo vya habari ni kumvunjia heshima.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment